Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI YAIMARISHA HUDUMA ZA KINGA DHIDI YA MAGONJWA MAENEO YA MIPAKANI.

Posted on: September 16th, 2025

Na WAF – Kigoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya imezidi kuimarisha mikakati ya kuikinga jamii ya wakazi wanaoishi maeneo ya mipakani dhidi ya milipuko ya magonjwa mbalimbali kwa kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa afya mipakani, maandalizi ya dharura na maboresho ya huduma katika vituo vya kutolea huduma.

Hayo yamebainishwa na Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, Septemba 15, 2025 mkoani Kigoma, wakati wa ziara yake mkoani hapa ambapo amesisitiza umuhimu wa kuendeleza juhudi za ufuatiliaji wa magonjwa ya mlipuko, kutoa elimu ya afya kwa jamii na kuhakikisha kila huduma ya afya inatolewa kwa ubora na kwa wakati.

Aidha katika ziara hiyo, Dkt. Grace alitembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni, Kituo cha Afya Gugu na Zahanati ya Kigoma kujionea namna huduma za zinavyotolewa baada ya kuongezeka kwa idadi ya watumishi, vifaa tiba, majengo na bidhaa za dawa na pia kufanya vikao na watumishi wa sekta ya afya. Akiwa katika vituo hivyo alipata pia nafasi ya kuongea na wananchi ili kupata mrejesho wa huduma zinazotolewa.

“Nichukue nafasi hii kuwakumbusha kila mmoja wenu analo jukumu la kuzingatia maadili na viapo vya taaluma na kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora, salama na yenye heshima,” amesema Dkt. Magembe.

Dkt. Magembe pia amesisitizia viongozi wa afya katika ngazi ya Mkoa, Halmashauri na waganga wafawidhi kwa pamoja kuimarisha usimamizi wa huduma za afya na kusimamia kikamilifu stahiki mbalimbali za watumishi.

“Viongozi wote tulioko hapa tunalo jukumu la kusimamia mazingira bora ya watumishi wa afya ili kuwaongezea morali ya kazi na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao,” amesisitiza.

Katika ziara hiyo Mganga Mkuu wa Serikali aliongozana na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Damas Kayera na Mkuu wa Huduma za Dharura Dkt. Micheal Kiremeji, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kigoma (Maweni) Dkt. Joseph Nangawe