Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI, WADAU WAKUTANA KUJADILI UDHAMINI ENDELEVU WA SEKTA YA AFYA KUELEKEA HUDUMA ZA AFYA KWA WOTE

Posted on: February 25th, 2025

Na WAF - Dodoma

Wizara ya Afya na wadau mbalimbali wa Sekta ya Afya nchini wamekutana Jijini Dodoma katika mkutano wa mwaka wa wataalam wa Mapitio ya Sekta ya Afya kujadiliana namna bora ya kuboresha huduma za Afya nchini.

Mkutano huo wa 24 pamoja na mambo mengine unaangazia Taarifa ya Mwaka ya Ufanisi wa Sekta ya Afya, kupokea taarifa ya mapato na matumizi ya sekta ya Afya kwa mwaka wa fedha 23/24, kupata taarifa ya kongamano la Bima ya Afya kwa wote na majadiliano ya Hali ya Udhamini wa Sekta ya Afya na kupitia mapendekezo ya Sera ya Vipaumbele vya sekta ya Afya vitakavyowasilishwa katika Mkutano wa pamoja wa Mapitio ya Sera ya Afya.

Akifungua Kikao hicho tarehe February 25, 2025 Jijini Dodoma Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seifu Shekalaghe amebainisha kuwa pamoja na mambo mengine Serikali imeanza kutekeleza sheria ya Bima ya Afya kwa wote ili kuhakikisha kila mtanzania ananufaika na huduma bora za Afya hapa Nchini.

Dkt. Shekalaghe amewataka wadau wote wa sekta ya Afya kuunga mkono utekelezaji wa Sheria hiyo kwani hadi sasa ni miaka 23 tangu ushirikiano wa Serikali na wadau katika kutekeleza afua mbalimbali za sekta ya Afya na serikali imekuwa ikisisitiza umuhimu wa utoaji huduma sawa kwa wote.

‘’Tumeimarisha ushirikiano ambao umekuwa chachu ya kupamba na changamoto zinazojitokeza hususani kuibuka kwa magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza hivyo ipo haja ya maandalizi ya wadau wote ikiwemo ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi ili kukabiliana na hali duni ya vitendea kazi, kuweka juhudi za pamoja ili kutoa huduma bora za Afya hapa Nchini,’’ ameongeza Dkt. Shekhalage.

Mkutano huo wa mwaka wa 24 wa wataalam wa Sekta ya Afya unaendelea kwa siku mbili Jijini Dodoma na kauli mbiu yake ni ‘’Kuelekea Udhamini Endelevu wa Sekta ya Afya Tanzania: Kipaumbele muhimu cha Bima ya Afya kwa Wote kufikia huduma ya Afya kwa Wote ifikapo 2030.’’