Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI, SHIRIKA LA HELLEN KELLER KUENDELEZA MAPAMBANO DHIDI YA TRAKOMA ARUSHA.

Posted on: August 7th, 2025

Na. WAF, Arusha


Wizara ya Afya kwa kushirikiana  na Taasisi ya Kimataifa ya Helen Keller inaendelea kutokomeza magonjwa yasiyopewa kipaumbele ikiwemo Trakoma kupitia Mradi wa usafi wa uso na uboreshaji wa mazingira unaotekelezwa katika Wilaya za Longido, Monduli na Ngorongoro Mkoani Arusha.


Helen Keller imekuwa mshirika wa karibu wa Serikali katika kuhamasisha mabadiliko ya tabia ya usafi na mazingira, ikilenga kupunguza maambukizi ya Trakoma,  kichocho na minyoo, ambayo yamekuwa tishio kwa jamii ya 

Kimasai.


Akizungumza wakati wa mapokezi ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Helen Keller International waliotembelea Mkoa wa Arusha Agosti 7, 2025 Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Bw. Daniel Loiruck amesema kuwa mradi huo umeongeza uelewa kwa watoto wa shule kuhusu umuhimu wa usafi wa uso na mikono, na pia umeongeza ujenzi wa vyoo na vituo vya kunawa mikono katika ngazi ya kaya.


“Tumeona mabadiliko ya kweli katika jamii zetu. Helen Keller imetusaidia kubadilisha mitazamo na tabia kuhusu usafi na mazingira, na hilo limechangia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza kasi ya maambukizi ya Trakoma,” amesema Bw. Loiruck


Amesema mradi huu umeendelea kuripotiwa katika vikao mbalimbali vya kitaalamu kama vile mikutano ya magonjwa yasiyopewa kipaumbele,  vikao vya usafi wa mazingira pamoja na mikutano ya robo ya mapitio ya Trakoma.


Aidha, Bw. Loiruck amesisitiza ushirikiano kati ya Helen Keller na Mkoa wa Arusha umechangia pia katika kuboresha hali ya afya na lishe ya jamii, na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo wakati wote.


“Tunaishukuru Helen Keller International kwa msaada wao endelevu, Ofisi yangu iko tayari kutoa usaidizi wowote utakaohitajika wakati wa ziara yenu ya kutathmini mradi katika Wilaya ya Monduli,” amesisitiza Bw. Loiruck.


Kwa upande wake Bi. Gigi Jorissen ameipongeza na kuishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwa nchi pekee inayofanyia kazi vipaumbele vya taasisi hiyo ambavyo ni kutokomeza magonjwa yasiyopewa kipaumbele, lishe pamoja na ugonjwa wa Trakoma.


“ Ujio wa wajumbe wa bodi ya wadhamini ni kuona namna kazi inavyofanyika na kuona kuzidi kuimarisha ushirikiano baina ya Taasisi ya Helen keller na Serikali ya Tanzania,” aliongeza Bi.Gigi Jorrisen.


Naye, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Edna- Chonge Ntulwe amesema utafiti wa athari za Trakoma uliofanywa na Wizara ya Afya mwaka 2021 ulionyesha kupungua kwa maambukizi hadi kufikia 14.6% kutoka 57.6% katika wilaya ya Longido, Monduli 9.1% kutoka 57.6% na kwa Ngorongoro 8.5% kutoka 52.5% kwa mwaka 2024 kabla ya kuanza kwa afua za utokomezaji ugonjwa huo.


Ziara ya wajumbe wa bodi ya wadhamini ya HKI inatarajiwa kuleta msukumo mpya katika utekelezaji wa miradi ya Afya ya jamii, hasa katika maeneo yanayoendelea kupambana na magonjwa ya kuambukiza yatokanayo na mazingira duni.