SERIKALI KUIMARISHA KLINIKI MAALUM KWA AJILI YA UGONJWA WA SELIMUNDU.
Posted on: February 21st, 2025
Na WAF - UYUI, TABORA
Mkurugenzi wa Idara ya Tiba Wizara ya Afya Dkt. Hamad Nyembea amesema Serikali iko mbioni kuanzisha na kuimarisha kliniki maalum za kukabilina na ugonjwa wa Selimundu kuanzia ngazi za chini.
Dkt. Nyembea amebainisha hayo Februari 20, 2024, Wilayani Uyui Mkoani Tabora wakati wa zoezi la usimamizi shirikishi ambalo linaendelea mkoani hapo na wataalam kutoka Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais - Tamisemi na Timu ya Usimamizi wa Afya Mkoa.
Dkt. Nyembea amesema tayari Serikali imeshaanza kugawa miongozo ya huduma za Selimundu kwa mtoa huduma katika baadhi ya halmashauri nchini, lengo likiwa ni kuboresha hali ya utoaji wa huduma za Selimundu hasa katika zahanati, na vituo vya afya vya pembezoni.
“Kwenye vituo vya afya ngazi ya chini watumishi watafundishwa namna ya kuwahudumia watoto na wote wenye uhitaji wa kupatiwa huduma za Selimundu lakini pia dawa za kuongeza damu na kutuliza maumivu zitatolewa ili wasipate madhira yanayotokana na ugonjwa wa Selimundu,” amesema Dkt. Nyembea.
Dkt. Nyembea ameongeza kuwa mkoa wa Tabora ni miongoni mwa maeneo yenye wagonjwa wa Selimundu na tayari kwenye hospitali na vituo kuna wagonjwa wanaohudhuria kliniki na kupatiwa huduma, jambo linaloisukuma zaidi Serikali kuanzisha kliniki maalum kwa ajili ya ugonjwa huo.
Kwa upande wake Daktari wa Magonjwa Yasiyoambukiza Dkt. Joseph Werema ambaye pia ni mratibu wa magonjwa yasiyoambukiza wilaya ya Uyui mkoani Tabora amesema wilaya hiyo imewatambua wagonjwa 756 wa selimundu kwa mwaka 2024 ambapo kati yao 398 wana umri chini ya miaka mitano (5) na 358 wanaumri zaidi ya miaka mitano (5).
Uyui imefikia hatua hiyo kupitia huduma za kliniki ya Selimundu ambazo zinatolewa katika hospitali ya wilaya ya Uyui na vituo vitatu vya afya vya Ilolangulu, Upuge na Igalula.