Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI KUENDELEZA TIBA ASILI, MBADALA KWA KUZINGATIA USALAMA, UBORA, MAADILI YA KITAALUMA.

Posted on: August 28th, 2025

Na WAF, Dodoma


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuendeleza tiba asili kwa kuhakikisha inakuwa sehemu ya mfumo wa huduma za afya kwa Watanzania wote, kwa kuzingatia viwango vya usalama, ubora na maadili ya kitaaluma.


Hayo yamebainishwa leo Agosti 29, 2025 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Khatibu Kazungu wakati akihitimisha Maadhimisho ya Siku ya Tiba Asili ya Mwafrika  jijini Dodoma,  akimwakilisha  Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.


Amesema tiba asili ni urithi wa taifa na mchango wake ni mkubwa katika kuboresha afya za wananchi na kukuza uchumi wa nchi.


“Tiba asili ni sehemu ya historia yetu na imekuwa chanzo kikuu cha huduma za afya kwa vizazi vingi. Serikali itaendelea kuwekeza katika utafiti, viwanda na mafunzo ili kuiendeleza,” amesema Dkt. Kazungu


Katika maadhimisho hayo, Serikali ameleza kuwa hatua kadhaa zimefikiwa ikiwemo kusajili zaidi ya dawa 141 kwa kuzingatia ubora na usalama, kuanzisha huduma jumuishi za tiba asili katika hospitali 14 za mikoa, na kukamilika kwa kiwanda cha kuzalisha dawa za tiba asili cha NIMR-Mabibo chenye mashine 39 za uzalishaji.


Aidha amesema, jumla ya wataalam wa tiba asili 64,000, vituo 2,100 na viwanda 75 vimesajiliwa hadi Juni 2024, hatua inayodhihirisha ukuaji wa sekta hiyo nchini.


Dkt. Kazungu amesema faida za uwekezaji katika tiba asili, utasaidia kuongeza ajira kupitia kilimo cha miti dawa, biashara na hata utalii wa tiba asili. 


Pia Dkt. Kazungu amewataka wananchi na halmashauri zote kuhakikisha mashamba ya miti dawa yanapandwa ili kulinda malighafi kwa matumizi endelevu.


Kwa upande mwingine, Serikali imewataka wataalam wa tiba asili kuzingatia miongozo rasmi katika utoaji wa huduma, kuepuka matangazo yasiyo rasmi kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii na kutokuhusisha taaluma yao na masuala ya kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao.


“Tuwajibike, tujiepushe na tamaa na tuendelee kuilinda taaluma ya tiba asili kwa misingi ya maadili, kwani lengo letu ni moja la  kukabiliana na adui maradhi,” amesisitiza.


Maadhimisho haya yamehusisha wataalam wa tiba asili kutoka mikoa mbalimbali, taasisi za utafiti, vyuo vikuu na wadau wa sekta ya afya na yamekuwa fursa ya kutafakari maendeleo yaliyofikiwa na mwelekeo wa baadaye katika sekta hiyo.