Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI, HELEN KELLER KUENDELEA KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA YA MACHO NCHINI

Posted on: November 1st, 2024

Na WAF - Mbeya

Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Helen Keller wameendelea kuboresha huduma za afya ya macho kwa ngazi ya msingi nchini.

Hayo yamebainishwa, Novemba Mosi, 2024 na Afisa kutoka Mpango wa Taifa wa Macho, Wizara ya Afya, Dkt. Greater Mande, wakati akihitimisha kambi ya macho iliyofanyika kwa siku saba wilayani Kyela, mkoa wa Mbeya.

Amesema Mpango huo unalenga kutoa huduma za uchunguzi wa macho, matibabu ya magonjwa yanayohusiana na macho, na kuhamasisha umma kuhusu umuhimu wa afya ya macho.

Dkt. Mande amesema kuwa kambi hiyo imefanyika kwa mafanikio kwani watu zaidi ya 400 wamefanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho, na zaidi ya wagonjwa watano wamepewa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya kwa huduma zaidi.

“Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Helen Keller tayari tumeshafanya kambi saba, na tunatarajia kufanya kambi nyingi zaidi ili wananchi wanufaike na huduma za macho.

Ametumia wasaa huo, kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi pindi wanapopata taarifa ya uwepo wa kambi za matibabu ndani ya mikoa yao.

Aidha, Dkt. Mande ameushukuru uongozi wa wilaya ya Kyela, mkoa wa Mbeya na Shirika la Helen Keller International kwa ushirikiano wao kwenye kampeni hiyo na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwafikishia wananchi huduma ya matibabu ya upasuaji wa mtoto wa jicho bure.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi kutoka Shirika la Kimataifa Helen Keller, Bw. Athuman Tawakal, amesema kuwa hii ni awamu ya kwanza ya kambi ya upasuaji wa mtoto wa jicho kufanyika Kyela, na lengo lilikuwa kuwafikia wagonjwa 420, ambalo limefanikiwa kwa kiwango kikubwa .

"Matibabu haya yote ni bure lengo ikiwa ni wananchi kunufaika na huduma za macho,” amesema Bw. Tawakal.