Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI, GLOBAL FUND KUSHIRIKIANA KUTEKELEZA AFUA ZA UKIMWI, KIFUA KIKUU

Posted on: February 23rd, 2025

Na WAF – DODOMA

Serikali itaendelea kushirikiana na Mfuko wa Dunia (Global Fund) katika utekelezaji wa afua za kupambana na UKIMWI na Kifua Kikuu nchini, ili kuboresha huduma za uchunguzi, matibabu, na kinga kwa wananchi.

Hayo yameelezwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Thomas Rutachunzibwa, Februari 21, 2025, wakati wa ziara ya kukagua miradi ya inayofadhiliwa na Global Fund mkoani Dodoma, ambaye aliambatana na timu ya wataalam kutoka Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais- TAMISEMI na ujumbe wa Global Fund kutoka Makao Makuu nchini Uswisi.

Dkt. Rutachunzibwa amesema juhudi inafanyika ya kugundua na kutoa taarifa za wagonjwa wapya wa Kifua Kikuu, hususan kwa makundi yaliyo katika hatari ya maambukizi.

Amesema, kwa mwaka 2024, lengo lilikuwa ni kugundua na kutoa taarifa za wagonjwa 1,084, ikiwa ni ongezeko la wagonjwa 86, ikilinganishwa na mwaka 2023 ambapo wagonjwa walikuwa 994.

Dkt. Rutachunzibwa amesema hadi kufikia mwisho wa mwaka 2024, halmashauri imefanikiwa kufikia asilimia 90.2 ya lengo hilo, huku ugunduzi wa wagonjwa wa watoto ukiwa asilimia 27.7 na ugunduzi kutoka kwa jamii ukiwa asilimia 29.2.

“Elimu na uhamasishaji kwa jamii ni muhimu ili kuongeza uelewa kuhusu kinga, uchunguzi wa mapema, na matibabu ya UKIMWI na Kifua Kikuu. Wananchi wanapaswa kufahamu dalili za magonjwa haya na kuchukua hatua za haraka wanapohisi wako katika hatari,” amesema Dkt. Rutachunzibwa.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwakilishi kutoka Global Fund Fund Dkt. Dany Karlos amesema Mfuko huo huo utaaendelea kushirikiana na Serikali kutekeleza afua mbali mbali za afya.

Dkt. Koros amesisitiza kuwa juhudi hizi zinapaswa kuendelezwa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya.