NGO ZA AFYA ZINGATIENI VIPAUMBELE VYA SERIKALI
Posted on: September 4th, 2024Na WAF, DODOMA
Mashirika yasiyo ya kiserikali yanayojihusisha na utoaji wa huduma katika sekta ya afya nchini yametakiwa kuwekeza nguvu kwenye vipambele vya serikali ikiwemo suala la bima ya afya kwa wote pamoja na uboreshaji wa huduma za afya.
Serikali imetoa kauli hiyo kupitia Naibu Waziri wa Afya Dk. Godwin Mollel, leo jijini Dodoma, wakati akifungua kikao cha mwaka kati ya serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotoa huduma kwenye sekta ya afya nchini.
Dk.Mollel amesema kwa sasa vipaumbele vya serikali kwa sekta ya afya ni bima ya afya kwa wote pamoja na uboreshaji wa huduma za afya kuanzia ngazi ya msingi hadi taifa.
“Moja ya kazi yenu ni kushirikiana na serikali ili kutekeleza vipaumbele vyake, hivyo basi kwa sasa vipaumbele vya serikali ni suala la bima ya afya kwa wote pamoja na kuboresha huduma za afya kwa wananchi”, amesisitiza Dkt. Mollel.
Ameeleza kuwa katika kipindi cha uongozi wa serikali iliyoko madarakani chini ya Rais Samia uwekezaji mkubwa umefanyika ndani ya sekta ya afya hivyo wadau hao hawanabudi kuunga mkono jitihada hizo.
“Hii inaamanisha kuwa uwekezaji uliofanywa na serikali ya wamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan wagonjwa wanagundulika mapema kabla hali haijawa mbaya wanapata tiba na kupona kulingana na uwekezaji kuanzia angazi ya msingi,”amesema Dkt. Mollel
Aidha, ameongeza katika kipindi cha miaka 60 iliyopita ni hospitali mbili tu ambazo ndio zilikuwa na kipimo cha CT Scarn, lakini hivi sasa kutokana uwekezaji uliofanya kipimo hicho kipo kwenye hospitali nyingi nchini.
Naye Mwenyekiti wa mashirika hayo yasiyo ya kiserikali yanayotoa huduma kwenye sekta ya afya nchini, Dickens Mbwana amesema lengo la kikao hicho ni kuanda mipango ya utekelezaji kulinga na vipaumbele vya serikali ili wanachi wapate Huduma stahiki.
“Tunaendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa serikali katika sekta ya afya ombi letu ni kuendelea kushirikishwa na serikali katika vipaumbele vyake na utekelezaji wa afua kadha ikiwemo mapambano dhidi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza”amefafanua Bw. Mbwana.