Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MUSWADA MAREKEBISHO SHERIA BIMA YA AFYA WAWASILISHWA

Posted on: March 4th, 2025

Na WAF, DODOMA 


Wizara ya Afya imewasilisha maboresho ya muswada wa Sheria ya Mfuko wa Bima ya Afya wa mwaka 2025 mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, ikilenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa watanzania.


Maelezo hayo yametolewa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama na kuihakikishia kamati hiyo kuwa Wizara itapokea maelekezo yote na kuyafanyia kazi kwa lengo la kuona mswaada huo unakuwa sheria.


Nayo Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imepongeza na kuitaka Wizara kuongeza juhudi za uhamasishaji kwa jamii ili kuleta uelewa juu ya umuhimu wa Bima ya Afya kwa Wote.


Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Elibariki Kingu, ameutaka Mfuko wa Bima ya Afya kutembelea mikoani na kukutana na makundi tofauti ya jamii ya wakulima, wafugaji, wachimbaji madini na mengine.


"Kufanya hivyo kutatoa fursa ya kuongeza wanachama wapya, hatua ambayo itaongeza idadi ya watu wenye uhakika wa kupata matibabu bora kupitia mpango wa Bima ya Afya," amefafanua Dkt. Mollel na kuongeza.


“Kuifikia jamii moja kwa moja ni njia bora ya kuhakikisha watu wengi zaidi wanaelewa faida za Bima ya Afya na hatimaye kujisajili. Hii itaongeza chachu ya kuboresha afya ya jamii na kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa mtu mmoja mmoja,” amesema  Mhe. Kingu.


Kwa upande wake, Dkt. Mollel ameahidi kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na wadau wote wa sekta ya afya ili kutekeleza mapendekezo ya kamati na kuimarisha huduma za afya kupitia mfuko huo, kwa maslahi mapana ya wananchi.