Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MONDULI YAPUNGUZA VIKOPE KWA ZAIDI YA ASILIMIA 80 KUPITIA MIKAKATI YA “SAFE”

Posted on: August 7th, 2025

Na, WAF Monduli


Wilaya ya Monduli imedhibiti kiwango cha maambukizi ya  ugonjwa wa vikope kutoka asilimia 57 mwaka 2006 hadi asilimia  9.1 mwaka 2022, kutokana na utekelezaji wa mkakati wa kimataifa ujulikanao kama 'Surgery, Antibiotics, Facial cleanliness and Environmental improvement (SAFE)'.


Hayo yamesemwa na Mratibu wa Magonjwa yasiyopewa Kipaumbele Wilaya ya Monduli Bi. Jubilate Temu wakati wa mapokezi wa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Kimataifa ya Hellen Keller walipotembelea wilaya ya Monduli na kufanya ukaguzi wa afua ya klabu za shule za maji, usafi binafsi na mazingira (SWASH) kwa shule ya msingi ya Orkeswa.


Bi. Jubilate amesema Halmashauri ya Wilaya kwa kushirikiana na wadau wa Shirika la Hellen Keller Inter ational (HKI), imeendesha upasuaji kwa waathirika, kusambaza dawa, kutoa elimu ya usafi wa mwili na mazingira, na kuhamasisha mabadiliko ya tabia kwa jamii nzima.


Mratibu huyo pia amesema,   watoto chini ya miaka 14 waliokuwa waathirika wakuu sasa wameanza kubadili maisha yao na kunufaika  kupitia elimu shuleni.


“Kupitia HKI, walimu 93 wa afya kutoka shule za msingi walipewa mafunzo ya kuhuisha klabu za shule za maji, usafi binafsi na mazingira (SWASH), kufundisha kupitia michezo ya karata zenye jumbe za usafi, na kuendesha vikao vya wazazi kwa lengo la kubadilisha tabia kwa familia, shule nyingi sasa zina vipindi rasmi vya SWASH,” amesema Bi. Jubilate.


Aidha, amefafanua kuwa viongozi wa vijiji nao wamehamasishwa kuhusu umuhimu wa kujenga vyoo bora na kuweka vifaa vya kunawa mikono, ufuatiliaji wa karibu shuleni umeendelea kuhakikisha kuwa elimu ya usafi inatekelezwa kwa vitendo.


“Halmashauri ya Monduli imeweka mkakati huu kwenye mpango wa kudumu kupitia idara ya afya na mradi wa WASH, kwa lengo la kuendelea kutokomeza kabisa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kama Trakoma, Kichocho na minyoo ya tumbo,” amesema Bi. Jubilate


Naye Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Hellen Keller International Bi. Eunice Reddick amesema Tanzania ni moja ya nchi  kati ya 20 zinazofadhiliwa na shirika hilo  kwa miaka 40 sasa ambapo mashirikiano yameendelea kuimarika baina ya Tanzania na  HKI.


“Taasisi ya Hellen Keller International inafanya kazi chini ya kanuni mbalimbali na moja ya kanuni hizo ilitokana na mwanzilishi wa Taasisi hii inayoenda sambamba na sera ya Serikali ya Tanzania inyotaka kila mwananchi kuwa na afya bora, pia Tanzania ni eneo muhimu kwetu kwa sababu ya kupiga kwao hatua katika kupunguza magonjwa yasiyopewa kipaumbele na magonjwa ya macho,” amesema Bi. Eunice.