Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MKOA WA IRINGA KINARA USHINDI WA JUMLA WA USAFI WA MAZINGIRA

Posted on: May 9th, 2024



Kibaha, Pwani

Mkoa wa Iringa umeibuka kidedea kwa ushindi wa jumla wa usafi na uhifadhi wa mazingira ambapo umezawadiwa gari aina ya Land Cruiser.

Akitangaza washindi wa usafi na usafi wa mazingira leo 9 Mei 2024 Kibaha, mkoani Pwani Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema Wizara ya Afya hufanya uhakiki wa vijiji ambavyo vimefikia kiwango cha juu cha usafi, zoezi ambalo linashirikisha vijiji ambavyo kaya zake zote zina vyoo, taasisi zilizopo katika Kijiji hicho na wananchi hawajisaidii ovyo katika maeneo ya wazi.

"Mwaka huu tumeongeza kundi moja la Mshindi wa Ujumla kwa Ngazi ya Mkoa, ambapo Mkoa uliofikia kiwango cha juu cha usafi kwa kuwa na Vijiji vingi vilivyofikia kiwango cha juu cha usafi ni Iringa ambao wanapata zawadi ya gari". Amesema Waziri ummy.

Kwa upande makundi mengine Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam kimeibuka mshindi wa kwanza wa usafi na mazingira na kupata cheti na Shilingi Milioni nne huku Chuo cha Kilimo Sokoine kikiibuka mshindi wa Pili na Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela kikiibuka mshindi wa Tatu.

Upande wa benki, Benki ya CRDB makao makuu Halmashauri ya jiji la Dar Es Salaam imeibuka mshindi na kupata zawadi ya cheti huku mshindi wa pili ni Benki ya NBC ya jijini Dodoma na mshindi wa tatu ni Benki ya NMB Rock City ya Wilaya na Ilemela jijini Mwanza.

Kundi la Hospitali za Wilaya mshindi wa kwanza ni Hospitali teule ya Migana Wilaya ya Misenyi, mshindi wa pili ni Hospitali ya mji wa Njombe na mshindi wa tatu Hospitali ya wilaya ya Kibosho Wilayani Moshi.

Kundi la Hospitali za Rufaa za Mikoa mshindi wa kwanza ni Hospitali Arusha Lutheran Medical Center (Seriani), mshindi wa pili Hospitali ya Rufaa ya Manyara huku mshindi wa tatu ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mount Meru Arusha.

Kundi la shule za msingi, mshindi wa kwanza ni shule ya Endabash ya wilayani Karatu, mshindi wa pili shule ya Kanikelele iliyopo Halmashuri ya wilaya Njombe huku mshindi wa tatu ni shule ya Idazinyi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.