Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MIFUMO YA WIZARA, MAABARA BINAFSI ISOMANE- KM AFYA

Posted on: October 13th, 2025

Na WAF - Dar es Salaam


Wizara ya Afya, imeagiza Bodi mpya ya 13 ya Maabara Binafsi za Afya kuhakikisha mifumo ya TEHAMA ya maabara binafsi   inasomana na mifumo ya Wizara ya Afya, kwa lengo la  kurahisisha usimamizi na uendeshaji wa huduma zao kwa uhakika  zaidi.


Agizo hilo limetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara  Afya Dkt. Seif  Shekalaghe leo Oktoba 13, 2025, jijini Dar es Salaam, wakati akizindua rasmi bodi hiyo mpya kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama.


Dkt. Shekalaghe amesema kusomana  kwa mifumo ya TEHAMA kutasaidia kuratibu na kusimamia vyema utoaji wa huduma za maabara binafsi, kufuatilia usajili wa maabara, pamoja na kutambua zile zilizositishiwa huduma au kufungwa kabisa.


“Ni matarajio yangu kuwa mtatekeleza majukumu yenu kwa weledi na ufanisi mkubwa, bila woga wa kuingiliwa katika maamuzi yenu, hakikisheni wawekezaji wanapata usajili bila vikwazo visivyo vya lazima,” amesema Dkt. Shekalaghe.


Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kusisitiza ushirikiano na sekta binafsi, ikizingatiwa kuwa takribani asilimia 40 ya huduma za maabara nchini zinatolewa na sekta binafsi,  hivyo kusaidia Serikali katika kuwahudumia wananchi.


Aidha, Dkt. Shekalaghe ameitaka bodi kuhakikisha maabara binafsi zinazoomba usajili zinakidhi vigezo vyote kabla ya kupatiwa vibali, sambamba na kufanya ukaguzi shirikishi wa maabara zote zilizosajiliwa ili kuhakikisha huduma bora zinatolewa muda wote.


“Maabara ni roho ya hospitali, hakuna daktari anayeweza kufanya kazi bila maabara, fanyeni ukaguzi shirikishi wa vifaa na utoaji wa huduma, na mtoe elimu kwa wamiliki na watumishi wa maabara binafsi,” ameongeza Dkt. Shekalaghe.


Aidha kiongozi huyo  amewapongeza wajumbe wa bodi iliyomaliza muda wao kwa miaka mitatu kwa kazi nzuri waliyofanya, ambayo imechangia kupunguza malalamiko kutoka kwa wadau na wananchi.


Awali, Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo, Dkt. Saitore Laizer, amesema bodi iliyomaliza muda wake imesajili maabara binafsi mpya 1,199, na kufanya jumla ya maabara zilizosajiliwa kufikia 4,353 na kuitaka bodi mpya kuendelea kusajili huku ikizingatia zaidi ubora wa huduma kuliko idadi pekee ya maabara.


Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa Bodi ya 13 ya Maabara Binafsi, ambae pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, Dkt. Hamad Nyembea ameahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Katibu Mkuu ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na zenye tija.


Bodi hiyo inaundwa na Wajumbe wengine ambao  ni Wakili Grace Thadei Komba kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Prof. Billy Ngasala - Chuo Kikuu cha Sayansi Shirikishi Muhimbili na Bi. Miriam Matonya kutoka Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii.


 Wengine ni Mkurugenzi wa Uchunguzi Wizara ya Afya Dkt. Alex Magessa, Prof. Jeremiah Seni kutoka Chuo Kikuu cha Afya ya Sayansi Shirikishi Bugando, Bw. Khamisi Ussi Khamisi - Mjumbe, Maabara ya Binafsi ya Dreem Iringa na Bw. Basilius Basil Kilowoko kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Benedict.