MASHINE ZA KUSAIDIA KUPUMUA 'CPAP' KUSAMBAZWA HOSPITALI ZOTE NCHINI
Posted on: September 20th, 2024
Na WAF - Dar Es Salaam
Serikali kupitia Wizara ya Afya imepanga kusambaza Vifaa Tiba kwa ajili ya kumsaidia kupumua mtoto mchanga mwenye tatizo la kupumua aina ya 'Continous Positive Airway Pressure' (CPAP) katika Hospitali zote zenye wodi maalum za watoto waliozaliwa kabla ya wakati (njiti).
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Septemba 19, 2024 wakati akikabidhi vifaa tiba hivyo baada ya kutembelea Bohari ya Dawa (MSD) ambavyo vimepokelewa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Dkt. Mohammed Mang'una kwa niaba ya Waganga Wakuu wote nchini.
Vifaa Tiba hivyo 130 vyenye thamani ya Tsh: Milioni 212,854,365/= vimenunuliwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kwa kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ili viweze kusaidia kupunguza vifo vya watoto hao.
"Tuendelee kunua mashine hizi ili ziweze kuenea kwenye vituo vyote vya Afya, Hospitali za Wilaya, tena sio moja angalau kila kituo kiwe na mshine hizi Tano, kwa sababu wanaweza wakapatikana watoto Watano kwa mara Moja, tuwasaidie watoto hawa wasipoteze maisha." Amesisitiza Waziri Mhagama
Amesema, watoto wanaozaliwa wakiwa na upungufu mdogo (njiti) kwa asilimia 80 wanakuwa na tatizo la kupumua kwa kuwa mapafu na viungo vingine vinakuwa havijakoma ambapo inapelekea kifo, lakini pia wanaweza kupata maambukizi kwa haraka kutokana na kinga yao kuwa chini.
Waziri Mhagama amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona jambo hilo ni muhimu na kulipa kipaumbele kwa kutoa maelekezo kwa MSD kununua vifaa hivyo ambavyo vitakwenda kusaidia kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa na tatizo ilo kwa asilimia 80.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bohari ya Dawa (MSD) Bw. Mavere Tukai amesema maagizo yote yaliyotolewa na Waziri wa Afya yatatekelezwa ikiwemo kuendelea na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia dawa, mifumo ya usafirishaji dawa ziomekane pamoja na kuendelea na uzalishaji wa bidhaa za dawa (Mask, Groves).