Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MAONI YA KAMATI YAFANYIWE KAZI ILI KUKAMILISHA MWONGOZO WA KITAIFA WA HUDUMA ZA AFYA NGAZI YA JAMII-DKT.GOWELLE.

Posted on: August 22nd, 2025

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Otilia Gowelle amesema ni muhimu maoni ya Kamati yakafanyiwa kazi kwa ufanisi katika kukamilisha Mwongozo wa Kitaifa wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii.



Dkt. Gowelle amebainisha hayo Mkoani Morogoro  wakati akiongoza  Kikao Kazi cha siku mbili cha Kukamilisha   Mwongozo wa Huduma za Afya ngazi ya Jamii kilichofanyika  kuanzia tarehe 21 hadi 22 Agosti 2025.


"Matarajio yetu sote ni kuhakikisha mwongozo huu muhimu unaanza kufanya kazi, hivyo ni muhimu kuyafanyia kazi maoni ya kamati kwani Mwongozo huu utakuwa na tija kubwa katika huduma za afya ngazi ya jamii"amesisitiza. 


Kikao kazi hicho kilijadili namna ya kukamilisha Mwongozo wa Kitaifa wa Huduma za afya Ngazi ya jamii kikihusisha wadau mbalimbali ikiwemo Amref Tanzania, UNICEF, WHO pamoja na Idara mbalimbali kutoka Wizara ya Afya. 


Lengo kuu lilikuwa kupitia na kupanua mwongozo ili kuhakikisha utekelezaji wake katika jamii unafanyika kwa ufanisi.


Ikumbukwe kuwa Kikao hicho kiliratibiwa na Wizara ya Afya, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma kwa kushirikiana na Ofisi ya Raisi-TAMISEMI  huku washiriki wote wakitoa maoni ya kujenga mwongozo wenye nguvu na unaotekelezeka.