Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MAGONJWA YA KICHOCHO NA MINYOO YAUNDIWA MKAKATI KUTOKOMEZWA TANZANIA

Posted on: August 25th, 2022Na. WAF - Dar es Salaam

Wataalamu mbalimbali wa Afya wamekutana na kujadiliana namna ya kuweka mkakati madhubuti wa kukabiliana na ugonjwa wa kichocho pamoja na minyoo ikiwemo kumezesha kingatiba nchini.

Afisa wa Programu ya Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kutoka wizara ya Afya Bw. Isaac Njau amebainisha hayo mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho Agosti 24, 2022 jijini Dar es Salaam.

Bw. Njau amesema mikakati na mbinu wanazojadiliana katika kikao kazi hicho zitaenda kusaidia wananchi na Serikali kwa kutokomeza Magonjwa hayo ifikapo 2030.

"Lengo letu kubwa ni kuchukua ushauri baada ya kugawa kinga tiba za Kichocho na minyoo ya tumbo kwa takriban miaka 15 ili kuweza kupata muelekeo wa jinsi ya kuendeleza kutoa kinga tiba hizi baada ya kuona maambukizi yamepungua kwa baadhi ya maeneo." Amesema Bw. Njau.

Aidha, amebainisha kuwa kuna baadhi ya maeneo ambayo bado maambukizi ya Magonjwa hayo yapo hivyo wanaendelea na mkakati ili yaweze kutokomezwa kabisa ifikapo 2030 kama alivyoagiza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Hata hivyo kikao hicho kimeweka mikakati ya kuendelea kumezesha kinga tiba kwa maeneo ambayo bado kuna maambukizi na maeneo yaliyositishwa kutolewa kwa kinga tiba hizo kuhakikisha wanasimamia masuala ya upatikanaji wa maji safi na kuendelea kutoa elimu kwa jamii.

Ikumbukwe kuwa hizi ni juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya ili kutokomeza Magonjwa hayo yaliyokuwa hayapewi kipaumbele baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. @samia_suluhu_hassan kusaini azimio la Kigali tarehe 27, Januari 2022 lengo ikiwa ni kujitoa kwa 100% kuhakikisha Tanzania inatokomeza Magonjwa hayo (NTDs) ifikapo 2030.