Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MAABARA BINAFSI ZAAGIZWA KUFUATA SHERIA NA MIONGOZO YA USAJILI

Posted on: March 15th, 2024



Na WAF - Dar es Salaam

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mohammed Mang'una, ametoa wito wa kusimamia kwa karibu maabara binafsi na kuzuia udanganyifu katika ajira ya watumishi wasio na sifa za kutosha ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Dkt. mang'una ameyasema hayo katika kikao cha mrejesho wa ukaguzi wa huduma za maabara binafsi katika mkoa wa Dar Es Salaam ambapo jumla ya maabara 112 zimebainika hazina usajili kati ya 476 zilizofanyiwa ukaguzi.

"Ni muhimu kusimamia maabara kwa karibu na kuepuka udanganyifu katika ajira ya watumishi wa maabara. Ni lazima tuwe na uhakika kwamba wanaofanya kazi ni wenye ujuzi na leseni husika". Amesema Dkt. Mang'una.

Kwa upande wake, Msajili wa Bodi ya Maabara Binafsi, Dominic Fwiling'afu, amesema kuwa ukaguzi huo umelenga kuhakikisha ubora wa huduma kwa wananchi kwa kuhakikisha kuwa maabara zinatoa huduma na majibu sahihi.

Hata hivyo, amebainisha kuwa katika ukaguzi huo, maabara 112 kati ya 476 hazikuwa zimesajiliwa na hivyo kukiuka taratibu, Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuzifungia maabara hizo hadi pale zitakapofuata taratibu za usajili.