Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

LIWALE YAPUNGUZA VIFO NA KUBORESHA HUDUMA YA MAMA NA MTOTO KUPITIA WAHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII

Posted on: March 12th, 2024



NA: WAF, Liwale-Lindi

Halmashauri ya Wilaya ya Liwale imeendelea kupunguza vifo vya Mama na Mtoto na kuboresha huduma hizo kwa kuwa na miundombinu rafiki ya huduma za afya na kupitia wahudumu wa afya ngazi ya jamii kwa kutoa elimu juu ya magonjwa mbalimbali.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, wakati wa ziara yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Liwale na kutembelea Kituo cha Afya Liwale mjini na Hospitali ya Wilaya Liwale kwa lengo la kukagua utoaji wa huduma za afya.

“Mhe Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania *Mhe* . *Dkt* . *Philip* *Mpango* alizindua mpango jumuishi wa wahudumu ngazi ya jamii tarehe 31 januari 2024, kwa lengo la kuwa na wahudumu hao nchi nzima. Maeneo yaliyopewa kipaumbele katika mpango huo ni Afya ya mama na mtoto, lishe, usafi wa mazingira, magonjwa yasiyo ya kuambukiza, magonjwa ya dharura na magonjwa ya kuambukiza ikiwemo Kifua kikuu, Malaria na UKIMWI”. Amesema Dkt. Magembe

Aidha Dkt. Magembe ameelezea umuhimu wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii katika kuelimisha jamii kuhusu hatari za magonjwa na jinsi ya kuzuia magonjwa mbalimbali kwani kwa kufanya hivyo kutaboresha afya za wananchi na jamii kwa ujumla.

“Kwa hakika, mchango wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii unaonesha umuhimu wao katika kuboresha afya ya jamii ya Liwale na kuendeleza ustawi wa kijamii Hatua hii ni dhamira nzuri ya kuboresha sekta ya afya na kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata huduma bora za afya kwakuwa kuna miundombinu rafiki ya huduma za afya”. Amesema Dkt. Magembe

Pia, amewapongeza watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Liwale kwa jitihada zao za kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kufika hospitalini wanapohisi dalili za magonjwa na kuachana na dhana potofu na kuwafata waganga wakienyeji.

Dkt. Magembe amewasisitiza watumishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Liwale kuendelea kuzingatia miongozo na viwango vya ubora wa huduma, huku akiwahimiza kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na za haraka.