Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

IMARISHENI HUDUMA STAHA ZINAZOZINGATIA UTU, MAWASILIANO BORA KWA WATEJA

Posted on: April 10th, 2025

Na WAF – Dodoma


Watumishi wa afya wamehimizwa kuimarisha utoaji wa huduma staha zinazozingatia utu wa mteja, heshima, maadili ya taaluma na mawasiliano bora.


Rai hiyo imetolewa Aprili 10, 2025 na Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Dkt. Rashid Mfaume, katika kikao cha uraghibishaji wa Kitita cha Huduma Staha kilichofanyika jijini Dodoma.


Dkt. Mfaume amesema kuwa Serikali imepiga hatua kubwa katika kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za afya, lakini mafanikio hayo hayatakuwa na maana iwapo huduma zitakuwa na ukakasi na kukosa staha kwa wateja.


“Nawakaribisha wadau kwa mikono miwili kushiriki kikamilifu katika kujadili na kupata uelewa wa kina kuhusu kitita hiki, ambacho kinalenga kubadilisha namna ya utoaji huduma kwa kuzingatia utu, heshima, na maadili ya taaluma ya afya,” amesema Dkt. Mfaume.


“Ninaamini kuwa baada ya zoezi hili la uzinduzi rasmi wa Kitita cha Huduma Staha, wadau wote mtashirikiana na Wizara ya Afya katika kujenga uwezo wa vituo vya kutolea huduma pamoja na watoa huduma, hasa katika ngazi ya msingi,” amesema Dkt. Mfaume.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga, Bi. Ziada Sellah, amesema kuwa ili kuhakikisha huduma za uuguzi na ukunga zinaimarika, ni muhimu kuzingatia utoaji wa huduma staha na mawasiliano madhubuti wakati wa kushughulika na mgonjwa.


“Hata kama dawa hazipo, inategemea unaongea kwa lugha gani. Kama utaweza kuwasiliana naye vizuri, mgonjwa huyo hatalalamika. Hivyo, nawahimiza watoa huduma za afya kufuata miongozo, kanuni na sheria za uuguzi na ukunga,” amesisitiza Bi. Ziada.


Naye, Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu, Bi. Grace Sheshua, amewataka watumishi wa afya kuzingatia mawasiliano bora, kuonesha huruma, na kujenga mazingira rafiki kwa wateja kama sehemu ya kuimarisha huduma katika ngazi zote za utoaji huduma.