Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

HUDUMA ZA UCHUNGUZI WA SIKOSELI, KISUKARI KWA WATOTO WACHANGA ZAZIDI KUIMARIKA NCHINI.

Posted on: March 15th, 2025

Na WAF - Mlimba, Morogoro

Huduma za uchunguzi wa Sikoseli na Kisukari aina ya kwanza kwa watoto wachanga wanapozaliwa zimezidi kuimarishwa katika maeneo ya pembezoni mwa miji.

Hilo limebainishwa Machi 14, 2025 Mkoani Morogoro ambapo timu ya Wataalamu toka Wizara ya Afya Kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tamisemi wakiongozwa na Mratibu wa Huduma za Sikoseli na Magonjwa ya Damu toka wizara ya Afya Dkt. Asteria Mpoto ilipofanya zoezi la usimamizi shirikishi na elekezi kwa Wilaya za Kilombero, Mahenge, Gairo na Ulanga.

Zoezi hilo limefuatia baada ya Mafunzo yaliyofanyika Tarehe 10 - 14 February 2025 katika Mikoa 7 na Halmashauri 50 kupata mafunzo juu ya uchunguzi wa Sikoseli na kisukari aina ya kwanza,
kwa lengo la kuhakikisha utekelezaji wa maazimio yaliyoazimiwa katika Mafunzo hayo ikiwemo kuanzishwa Kwa kliniki katika vituo vya kutolea huduma za Afya.

Kwa sasa tayari sehemu kubwa ya hospitali za Halmashauri nchini zimeshaanzisha na kuendesha kliniki hizo walau mara mbili kwa wiki jambo ambalo linasaidia kutambua wagonjwa wapya na kuwapa matibabu wakiwa katika hatua za awali.

Mratibu wa huduma za Siko Seli na magonjwa ya damu toka Wizara ya Afya Dkt. Asteria Mpoto amesema lengo la Serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha huduma zinasogezwa Kwa wananchi ili kuwarahisishia waweze kupata matibabu Kwa urahisi.

Aidha, Huduma hizo zinapatikana katika Hospitali za Wilaya na Vituo vya Afya badala ya kwenda kwenye hospitali za rufaa za Mikoa na Hospitali za Rufaa za Kanda.