Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

HUDUMA ZA DHARURA ZAOKOA MAISHA YA WANANCHI MKOANI SIMIYU

Posted on: February 23rd, 2024



NA: WAF - SIMIYU

Serikali ya awamu ya sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuimarisha sekta ya afya kwa kujenga majengo ya Huduma za dharura 101 katika maeneo mbalimbali nchini ambapo Mkoa wa Simiyu ni kati ya Mikoa iliyofaidika.

Hayo yamebainishwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe Februari 23, 2024, wakati wa ziara yake akiwa Mkoani Simiyu alipotembelea Hospitali ya Wilaya Bariadi na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Simiyu kujionea mafanikio ya majengo hayo tangu kuanzishwa kwake ambapo wagonjwa pamoja na majeruhi zaidi ya 200 wameshahudumiwa kwenye hospitali hizo mbili.

Katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Simiyu, Dkt. Magembe alijionea namna jengo la dharura linavyoweza kuhudumia majeruhi wengi kwa pamoja (Mass Casualities) na kuwapanga kutokana uhitaji wa haraka wa huduma (Triaging) ili kuokoa maisha kwa haraka.

“Jengo la huduma ya dharura limekuwa na umuhimu mkubwa tangu kuanza kutoa huduma mwezi Agosti 2023. Mpaka kufikia Februari 2024, jumla ya wagonjwa 191 wa dharura wamepatiwa huduma katika jengo hili. Hii imepunguza mzigo kwa wagonjwa ambao hapo awali walilazimika kusafiri umbali mrefu kwenda kupata huduma hiyo”. Amesema Dkt. Magembe.

Kwa upande wake Mkuu wa huduma za dharura Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu Dkt. Juma Munna amesema Hospitali hiyo inapokea dharura zote kati ya 40 hadi 50 kwa siku wakiwemo watoto na watu wazima.

"Utaona kuna dharura za ajali, upasuaji, walioumia kichwani, dharura za magonjwa ya ndani na mlipuko. Tunawachukua taarifa zote za muhimu na vipimo vya dharura wakiwa hapahapa, hadi wakihitaji X-ray tunayo mashine inayotembea (Mobile X-ray) kwa wale walioumia sana na hawawezi kusafirishwa kirahisi kwenda jengo la mionzi". amesema Dkt. Juma Munna.

Nae Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Halmashauri ya Bariadi Dkt. Flavian Jacob Rweyungura amesema Haya ni mapinduzi makubwa katika kuokoa maisha ya wananchi kwa kuwapunguzia wananchi umbali wa kupata huduma.