Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

HUDUMA ZA CT SCAN KATIKA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA IRINGA KUANZA KUTOLEWA SEPTEMBA 15, 2022

Posted on: August 12th, 2022

Na Englibert Kayombo, WAF- Iringa. 

Kuanzia tarehe 15 Septemba huduma za uchunguzi na matibabu ya kibingwa kwa kutumia CT SCAN zitaanza kutolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. @UmmyMwalimu leo alipokuwa akizungumza na wananchi wakazi wa Mkoa wa Iringa kwenye Mkutano wa hadhara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika uwanja wa Samora uliopo Iringa Mjini.

Waziri Ummy amesema kuwa hakutokuwa na haja tena kwa wakazi wa Iringa kwenda mbali Mikoa ya Dodoma au Mbeya kufuata huduma za CT -SCAN.
Katika kuchukua hatua za kusogeza karibu zaidi huduma kwa wananchi, Waziri Ummy amesema kuwa amepokea ombi kutoka kwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa Mhe. Ritha Kabati la kupeleka Daktari wa Mifupa katika Hospitali ya Rufaa ya Iringa na ambapo Waziri Ummy ameahidi kupeleka Daktari Bingwa wa Mifupa katika Hospitali hiyo.

“Niko hapa na Rais wangu Mhe Samia Suluhu Hassan, nataka niwaahidi wanairinga tutaleta Daktari Bingwa wa Mifupa katika Hospitali yetu ya Rufaa ya Iringa ili tuwapunguzie safari za kwenda Dodoma au Mbeya kwa ajili ya kupata huduma za Daktari Bingwa wa Mifupa” amesema Waziri Ummy Mwalimu