Customer Feedback Centre

Ministry of Health

HUDUMA MKOBA KUBORESHA UTAMBUZI WA MAGONJWA YA MACHO

Posted on: April 11th, 2025

Na WAF, Morogoro


Wataalam na Waratibu wa huduma za  Macho wa mikoa wameweka malengo ya kuwa  na mikakati ya kuboresha huduma za macho nchini kwa kutumia huduma mkoba.


Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Dkt. Alphonce Chandika Aprili 11, 2025 mkoani Morogoro katika kikao cha mwaka cha wataalam na waratibu wa huduma za macho wa mikoa.


Dkt. Chandika amesema wataalam hao wamekuja na mikakati ya kuibua wagonjwa kwenye jamii kwa kufanya utambuzi wa haraka kwa huduma mkoba katika maeneo mbalimbali nchini," amesema Dkt.Chandika.


"Takwimu zinaonesha matatizo ya uoni hafifu kwa wananchi yanasababishwa zaidi na mtoto wa jicho, hivyo madaktari hao wameweka mikakati ya kutambua magonjwa mapema kwa kuwafikia wananchi katika maeneo yao," amesema Dkt. Chandika.


Aidha Dkt. Chandika amewapongeza  madaktari hao kwa kufanya kazi kubwa hasa ya kuibua magonjwa ambayo yangeweza kusababisha  upofu.


Kwa upande wake Meneja Mpango wa Taifa wa Huduma za Macho Dkt. Bernadetha Shilio amesema wataalam hao wamepata fursa ya kushirikishwa kutoa maoni yao kwenye miongozo inayoendelea kuandaliwa ili kusaidia uboreshaji wa huduma za macho nchini.


"Kupitia kikao hicho wananchi watarajie huduma zitakazotolewa kupitia miongozo hii zitakuwa ni bora na zitawafikia wote mahali walipo," amesema Dkt. Shilio.


Naye Mratibu wa Huduma za Macho kutoka mkoa wa Morogoro Dkt. Wahida Mtiro ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuboresha huduma za macho  kwa kuhakikisha huduma hizo zinapatikana nchi nzima katika ngazi zote za vituo vya kutolea huduma za Afya.