Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

HOSPITALI YA RUFAA MKOA WA SINGIDA KUENDELEA NA UJENZI WA HOSPITALI BAADA YA KUSIMAMA KWA MUDA MREFU

Posted on: February 25th, 2024



Serikali imeutaka uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida kuhakikisha wanaendelea na mradi wa ujenzi wa mradi wa jengo la Ghorofa 3 na wanakamilisha ujenzi wa jengo la EMD (Emergency Department) na ICU (Intensive Care Unit)

Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, akiwa katika ziara yake ya kukagua miradi ya ujenzi katika sekta ya Afya nchini huku akisisitiza dhamira ya Serikali katika kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya, na kufanya huduma hizo ziwe karibu zaidi na wananchi.

"Kwa kuwa jengo la EMD na ICU ni majengo yanayohitajika sana katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa singida, Uongozi wa Hospitali hakikisheni taratibu za kuwapata mafundi zinakamilika mapema ili wafike site mwanzoni mwa Mwezi Machi, 2024”. Amesema Dkt. Magembe

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa Singida Dkt. David Mwasota amesema Ghorofa hilo likikamilika litatoa huduma ya Upasuaji wa kawaida pamoja na mifupa, Maabara, wodi za kulaza wagonjwa, wodi ya watoto, wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum na ofisi mbalimbali.

Kutokana na umuhimu wa jengo hilo Naibu Katibu Mkuu ameagiza hatua za haraka zichukuliwe kufanikisha ujenzi huu ikiwa ni Pamoja na kumpata Mshauri elekezi kwa ajili ya jengo hilo pamoja na kupata mafundi wa kumalizia jengo la EMD na ICU

Dkt. Magembe amemtaka Mkurugenzi wa Tiba Prof. Pascal Ruggajo kusimamia uandaaji wa Mpango kazi wa utekelezaji wa majengo yote matatu huku akimuelekeza Mkurugenzi Msaidizi wa bajeti na mipango wizara ya afya kuhakikisha fedha zilizotengwa kwa miradi hii zinatumika kabla ya mwaka wa fedha kuisha ili kuzuia kusuasua na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa wakati na kwa ufanisi.