HOSPITALI SABA ZATEULIWA KUTEKELEZA HUDUMA ZA UTALII WA MATIBABU
Posted on: October 30th, 2024Na WAF-Dodoma
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema Serikali imeteua Hospitali saba kutoa huduma za tiba za kitalii, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuboresha na kuimarisha sekta ya afya nchini.
Dkt. Mollel amesema hayo leo Oktoba 30, 2024 bungeni Jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Prof. Patrick Alois Ndakidemi mbunge wa moshi vijijini ambaye aliuliza “Je, Serikali imechukua hatua gani za kuimarisha tiba za kitalii kutokana na kuimarika kwa huduma za afya katika Hospitali za Rufaa”.
Dkt. Mollel amesema kuwa katika Hospitali saba zilizoteuliwa tano kati ya hizo ni za umma, ikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Mifupa Muhimbili, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, na Hospitali ya Benjamin Mkapa. Hospitali mbili za binafsi ni SAIFEE na AGAKHAN.
Dkt. Mollel amefafanua kuwa uwekezaji huu unahusisha kununua vifaa tiba vya kisasa na kuimarisha miundombinu ya Hospitali hizi ili ziweze kutoa huduma za hali ya juu kwa wagonjwa wa ndani na wa kimataifa kwani Serikali imeweka mkazo katika kusomesha wataalamu wa afya kwenye ngazi ya ubingwa na ubingwa bobezi ili kuimarisha utoaji wa huduma bora na kuendana na viwango vya kimataifa.
Aidha, Dkt. Mollel amesema kuwa Serikali inaendelea kuimarisha huduma za afya katika Hospitali za kanda kwa kuongeza vifaa na miundombinu katika maeneo yenye uhitaji mkubwa kama vile Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mtwara pamoja na kujenga Hospitali ya Kanda ya Kigoma ikiwa na lengo la kuimarisha huduma za afya pamoja na tiba utalii kwa nchi za jirani na maeneo hayo.
Hatua hizi zinalenga sio tu kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa ndani, bali pia kuleta mafanikio makubwa katika sekta ya utalii wa tiba kwa kuvutia wagonjwa kutoka nchi jirani na maeneo ya mbali, hivyo kusaidia kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta ya afya.