Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

HADI NOVEMBA 10 MIFUMO YOTE YA AFYA ISOMANE KURAHISHA HUDUMA ZA TIBA KWA WAGONJWA

Posted on: September 4th, 2024

Na WAF - Dodoma


Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ametoa maelekezo kwa Idara ya Tiba Wizara ya Afya kuhakikisha wanasimamia mifumo yote ya Afya isomane ili kurahisha huduma za Tiba kwa wagonjwa ikiwemo rufaa za ndani na nje ya nchi. 


Waziri Mhagama amesema hayo leo Septemba 4, 2024 wakati wa kikao cha ndani na Idara ya Tiba Wizara ya Afya kwa lengo la kujitambulisha, kutambua majukumu ya Idara hiyo pamoja na kujadili utendaji kazi wa Idara hiyo. 


"Ni muhimu sana kuwa na mifumo iliyo imara na tumekubaliana hapa, hadi kufikia novemba 10 mifumo ya Afya isomane ili kumrahishia mgonjwa kupata huduma za Tiba kwa haraka ikiwemo huduma za kibingwa za rufaa ndani na nje ya nchi pamoja na kuwepo kwa taarifa za mgonjwa." Amesisitiza Waziri Mhagama


"Tukumbuke kazi zote tunazozifanya ni kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa yeye ndiye anaesimamia watumishi wote na tukifanya vizuri katika kazi zetu tutakua tunamuheshimisha na kutekeleza maagizo yake." Amesema Waziri Mhagama 


Aidha, Waziri Mhagama amesema pamoja na kuwepo kwa mifumo hiyo ya Afya ambayo inasomana, kuwe na mfumo utakaosaidia kufuatilia taarifa za dawa za tiba asili. 


Mwisho, Waziri Mhagama amewapongeza watumishi wa Idara ya Tiba kwa kufanya kazi kubwa na nzuri ya kuwahudumia wananchi hasa katika huduma za kibingwa na kuwataka waendelee kufanya kazi hiyo kwa bidii, kwa pamoja na kupendana ili tupate matokeo chanya. 


Kwa upande wake Mkurugenzi wa huduma za Tiba Wizara ya Afya Dkt. Hamad Nyembea wakati akiwasilisha taarifa ya Idara ya Tiba kwa Waziri wa Afya amesema jitihada zinaendelea za kuhakikisha huduma zote za Afya zinapatikana nchini. 


"Tunajitahidi huduma zote zipatikane ndani ya nchi lakini kama mgonjwa atalazimika kwenda nje ya nchi kuna rufaa zinatolewa katika Hospitali zetu za ndani kwa lengo la kuhakikisha mwananchi anapona." Amesema Dkt. Nyembea


Pamoja na mambo mengine Dkt. Nyembea amesema Wizara ya Afya inatarajia kujenga Hospitali kubwa ya kisasa kwa ajili ya kutoa huduma za tiba asili nchini.