Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

DKT. MPANGO AAGIZA WIZARA YA AFYA NA TAMISEMI KUZIWEZESHA IDARA ZA AFYA

Posted on: May 9th, 2024



Na WAF - Kibaha, Pwani

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Phillip Mpango ameziagiza Wizara ya Afya na OR-TAMISEMI kuziwezesha idara za Afya kuanzia ngazi ya Halmashauri za Manispaa, Miji na Majiji ili waweze kuimarisha mifumo ya kutambua, kudhibiti na kukabiliana na magonjwa ya milipuko.

Dkt. Mpango amesema hayo leo 9 Mei, 2024 Kibaha Mkoani Pwani wakati akizindua Kampeni ya Mtu ni Afya inayolenga kujikita zaidi katika huduma za kinga ikiwemo usafi wa mazingira badala ya kuwekeza kwenye tiba.

Dkt. Mpango amesema ikiwa idara hizo zitawezeshwa zitaweza kujengewa uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko ikiwemo kuimarisha mifumo ya kutambua, kudhibiti na kukabiliana na magonjwa.

“Endapo idara hizi zitawezeshwa licha ya kubaini na kukabiliana na milipuko pia zitaweza kufanya tafiti kuhusu magonjwa mbalimbali ili kubaini jinsi yanavyosambaa, vihatarishi na tiba yake”. Amesema Dkt. Mpango.

Aidha, ametoa rai kwa Halmashauri zote kuwatumia wahudumu wa ngazi ya jamii ambao watawezesha kufikiwa sehemu kubwa ya jamii lakini kuchochea mabadiliko ya tabia za wananchi na kubakikisha usawa na urahisi wa utoaji wa huduma.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema Serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Afya imekuwa ikiboresha huduma za afya kwa watanzania kwa kutilia mkazo masuala mbalimbali ikiwemo huduma za Afya kinga ili kudhibiti na kuzuia magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza yanayoweza kutokea kwenye jamii.

“Niwakumbushe kuwa, Kampeni ya Usafi wa Mazingira awamu ya kwanza (2012-2015) ilizinduliwa na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wakati ule, Awamu ya Pili (2016-2022) ya Kampeni hiyo ambayo ilikuwa na kauli mbiu isemayo NYUMBA NI CHOO ilizinduliwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye alikuwa Makamu wa Rais kwa wakati huo”. Amesema Waziri Ummy.