Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

DKT. MAGEMBE AAGIZA UJENZI WA CHUO CHA UUGUZI NA UKUNGA NACHINGWEA KUKAMILIKA IFIKAPO SEPTEMBA 2024

Posted on: March 13th, 2024



Na: WAF, Nachingwea-Lindi

Naibu Katibu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, ameagiza kukamilika kwa ujenzi wa jengo la Chuo cha Uuguzi na Ukunga Nachingwea ifikapo mwezi Septemba 2024, na kuanza kudahili wanafunzi mwezi Oktoba kwa lengo la kufundisha na kupunguza changamoto ya watumishi katika Mkoa wa Lindi.

Dkt. Magembe ameyasema hayo wakati wa ziara katika Mkoa wa Lindi kwa lengo la kukagua miradi ya ujenzi na hali ya utoaji huduma za afya.

Aidha, Dkt. Magembe amemtaka Mhandisi wa miradi kutoka Wizara ya Afya Eng. Johnson Kamala kuandaa Mpango wa utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi ukionyesha kila hatua ya ujenzi, muda na wahusika wote kwa ajili ya ufuatiliaji wa karibu kwa lengo la kuhakikisha unakamilika ndani ya muda uliopangwa huku akisisitiza umuhimu wa usimamizi wa karibu ili kuhakikisha ubora na ufanisi wa mradi huo.

“Uwepo wa chuo karibu na Hospitali itasaidia kupunguza adha na changamoto ya upungufu wa watumishi katika Hospitali ya Halmashauri Nachingwea pamoja na Halmashauri za jirani, kufikia Septemba kiwe kimekamilika na udahili ufanyike. Amesema Dkt. Magembe

Naye Mhandisi wa Wizara Eng Kamala amemuhakikishia Naibu Katibu Mkuu kuwa changamoto zilizokuwepo zimetatuliwa na taratibu zote za kimkataba zimekamilika na kuanzia tarehe 18/03/2024 Mkandarasi wa Jengo hilo atarejea eneo la ujenzi ili kuendelea na kazi.

Dkt. Magembe amesema ni azma ya serikali ya awamu ya sita kuboresha sekta ya afya kwa kuhakikisha upatikanaji wa watumishi wenye ujuzi na weledi watakaochangia maboresha katika sekta ya afya na kuimarisha ustawi wa jamii.