AFYA CALL CENTER YAPATA TUZO YA “DIGITAL HEALTH EXCELLENCE”
Posted on: August 11th, 2025
Na WAF, Zanzibar
Kituo cha kupokelea simu na kujibu hoja za wananchi kuhusu masuala ya afya cha (199 Afya Call Center) kimetwaa tuzo ya Ubora wakati wa hafla ya Afya Kidijitali (Award in Digital Health Excellence) kwenye maonesho ya East Africa Youth Business and Investment Expo yaliyofanyika hivi karibuni visiwani Zanzibar.
Tuzo hiyo imekabidhiwa Agosti 10, 2025 na Mke wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Mariam Mwinyi, na kupokelewa na Dkt. Otilia Gowelle, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga, Wizara ya Afya kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya.
Afya Call Center imetambuliwa na kupewa tuzo hiyo kutokana na mchango wake mkubwa kwa jamii kupitia huduma za kidijitali zinazowawezesha wananchi kupata elimu, taarifa sahihi, ushauri wa kitaalam na uelewa kuhusu masuala mbalimbali ya afya bila kujali umbali au changamoto za usafiri. Huduma hizi zimekuwa msaada mkubwa hasa wakati wa majanga ya kiafya, kampeni mbalimbali za afya, pamoja na ufuatiliaji wa magonjwa.
Tuzo hiyo pia ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali kupitia Wizara ya Afya kutumia teknolojia za kisasa katika kuboresha upatikanaji wa huduma na taarifa za afya, sambamba na ajenda ya taifa ya mageuzi ya kidijitali ili kufikia azma ya ufikiaji wa huduma za afya kwa watu wote (Universal Health Coverage).