Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAZIRI UMMY AZINDUA MAABARA YA PATHOLOJIA KATIKA HOSPITALI YA MOUNT MERU

Posted on: December 30th, 2023

Na. WAF - Arusha

Katika kuendelea kuboresha Sekta ya Afya nchini, Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amezindua maabara ya Patholojia iliyopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru kwa lengo la kusaidia kurahisisha uchunguzi wa magonjwa mbalimbali ikiwemo ya upimaji wa vinyama ambavyo vinatokana na uvimbe katika sehemu mbalimbali za mwili.

Waziri Ummy amefanya uzinduzi huo leo Disemba 30, 2023 baada ya kufanya ziara yake ya kukagua huduma za Afya zinazotolewa katika Hospitali hiyo pamoja na upatikanaji wa dawa.

“Nipongeze hatua hii na maelekezo yangu kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya kupitia kwa Mganga Mkuu wa Serikali, turuhusu Hospitali za Rufaa za Mikoa kuanza kutoa huduma za kemia tiba kwa wagonjwa Saratani.” Amesema Waziri Ummy

Amesema, hatua za awali zifanyike ikiwemo kufanya ukaguzi kwa kuangalia wodi, vitanda vingapi vinatakiwa na kama Hospitali itakuwa na vigezo vyote, huduma hiyo ianze.

Katika hatua nyingine, Waziri Ummy ametoa pongezi kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha kwa kutoa huduma bora za Afya na kuzingatia usafi wa mazingira na kupunguza malalamiko zaidi ya 90% kutoka kwa wananchi pamoja na watumishi katika Hospitali hiyo.

Waziri Ummy ameridhishwa na huduma zinazotolewa katika Hospitali hiyo baada ya kutembea na kujionea wodi mbalimbali ikiwemo wodi ya wazazi, wodi ya watoto njiti (NICU), wodi ya uangalizi maalum (ICU) pamoja na CT-Scan.

“HospitalI nyingine za Rufaa za Mikoa ziige mfano wa huduma zinazotolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru pamoja na kuzingatia usafi wa mazingira ili kuepuka magonjwa mengine ya milipuko.” Amesema Waziri Ummy

Mwisho, Waziri Ummy amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kununua vifaa pamoja na vifaa tiba ili wananchi wapate huduma ndani ya Tanzania na kupunguza Rufaa za nje ya nchi.