Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WATOTO ZAIDI YA MILIONI 8 NCHINI KUPATIWA CHANJO YA SURUA RUBELLA

Posted on: February 16th, 2024



Na.WAF, Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya imezindua kampeni ya Kitaifa ya Chanjo ya Surua Rubella ambapo kwa nchi nzima wanatarajia kuwafikia watoto 8,908,810 wenye umri chini ya miaka mitano.

Hayo yamebainishwa Leo Jijini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Tumaini Haonga akimuwakilisha Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu katika uzinduzi wa kampeni ya chanjo Kitaifa Februari 15, 2024 katika maeneo mbalimbali nchini na inatarajiwa kumalizika Jumapili Februari 18, 2024.

Dkt. Haonga amesema kuwa lengo la kampeni hii ni kuhakikisha wanazuia kuenea kwa ugonjwa surua na rubella pamoja na kuongeza kinga kwa walengwa.

Dkt. Haonga amesisitiza usimamizi wa chanjo hiyo kutokana na umuhimu wake kwani inaongeza kinga kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Ameongeza kuwa zaidi ya vituo 7,373 katika maeneo mbalimbali nchini vimetengwa kwa ajili ya kuhakikisha wanatoa Huduma hiyo kikamilifu ili kuweza kufikia lengo waliojiwekea..

Hata hivyo amewataka Wakuu wa Mikoa,Wilaya na Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanasimamia kikamilifu zoezi kuwapatia chanjo watoto wenye umri kuanzia miezi tisa mpaka 59 (chini ya miaka mitano)

"Niwaombe wazazi kuitumia fursa hii kuwapeleka watoto wao waweze kupatiwa chanjo kwani ni muhimu kwa watoto kupata chanjo hiyo,"ametoa wito Dkt. Haonga.

Dkt. Haonga amesema wamepata mrejesho tangu kuanza kwa chanjo kwa zoezi hilo katika maeneo mbalimbali wazazi wamejitokeza kwa wingi na wanaendelea kujitokeza ili kulinda afya za watoto wao.