Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WATAKIWA KUTOA MAONI, USHARI, KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA YA MACHO

Posted on: October 8th, 2025

Na WAF - Morogoro

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Best Maghoma amewataka wajumbe wa kikao kazi cha Kamati ya ya Afya ya Macho kujadiliana kwa kina, kutoa maoni, ushauri kwa Wizara ya Afya ili kuendelea kutoa huduma bora za macho kwa wananchi kwa kuwa kazi hiyo ni kubwa ya kujadili masuala muhimu kwa taifa.

Dkt. Maghoma amesema hayo leo Oktoba 07, 2025 akimwakilisha Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya Dkt. Hamad Nyembea katika kikao kazi cha Kamati ya Afya ya Macho kilichoandaliwa na Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Huduma za Macho nchini.

"Kikao hiki ni kikao muhimu na cha kitaalam, naamini ni nafasi nzuri ya kuwa na mijadala mbalimbali ya kuona ni namna gani tunaweza kuongeza huduma hizi za matibabu ya macho na kwa wadau wetu tunawashukuru kwakuwa mambo ni mengi lakini mmeweza kutenga muda wenu," amesema Dkt. Maghoma.

Amesema, magonjwa yanayohusiana na macho ni kati ya magonjwa ambayo yapo ndani ya magonjwa kumi yanayowasumbua Watanzania, watalaam wanavyoendelea kupatikana ndipo idadi ya wagonjwa inapozidi kuongezeka kwakuwa watakuwa na uwezo zaidi wa kuweza kuwafikia wagonjwa.

Aidha, Dkt. amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuongeza wataalam hao pamoja na kuongeza vifaa katika vituo vya ngazi mbalimbali ambavyo vinawezesha kufanyika kwa matibabu ya wagonjwa wa macho kwa usahihi.

"Tunatambua mchango wa wadau kwa kutoa huduma hizi za matibabu ya macho katika kambi mbalimbali zinazofanyika nchini, wananchi wengi wanatoka kufuata huduma hizo ambazo zinaonesha kuwa mahitaji bado ni makubwa katika jamii," amesema Dkt. Maghoma.