Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WATAALAMU WA MAABARA WAASWA KUJIENDELEZA KIELIMU

Posted on: October 26th, 2023

Na. WAF - Dodoma 


Serikali kupitia Wizara ya Afya ipo tayari kuwafadhili wataalam wa Afya ikiwemo wataalam wa Maabara watakaokuwa tayari kujiendeleza kielimu ili kukuza ujuzi katika fani zao. 


Mkurugenzi wa Mafunzo na Maendeleo ya Rasilimali watu Dkt. Saitori Laizer amesema hayo leo Oktoba 27, 2023 wakati akiongea na Wataalam watarajali wa Maabara kwenye semina elekezi ya kwenda kuanza mafunzo ya utarajali katika vituo vya kutolea mafunzo. 


“Tumieni fursa ya kujiendeleza kielimu ili muongeze ujuzi katika fani zenu na Serikali kupitia Wizara ya Afya chini ya Raisi wetu Dr. Samia Suluhu Hassan ipo tayari kuwafadhili wataalam wa Afya kwa wale ambao wana nia na wapo tayari kujiendeleza”. Amesema Dkt. Saitori 


Aidha, Dkt. Saitori amewaasa watarajali hao kwenda kufanya mafunzo hayo kwa kuzingatia nidhamu na kujituma kwa kuwa ndio fursa pekee ya kujijengea uzoefu wa taaluma yao kwa vitendo baada ya kuhitimu. 


Pia, amewahimiza kwenda kufanya kazi kwa kuzingatia weledi wa Taaluma yao ikiwemo kufuata Miiko na Maadili ya taaluma ya Maabara kwa kuwa taaluma hiyo ni kama hakimu ambae ni mwamuzi wa mwisho kuhusiana na matibabu ya mgonjwa kutokana na majibu anayoyatoa kwa Daktari.


“Fanyeni kazi kwa kufuata miongozo yenu ya Taaluma ya Maabara ambapo ni pamoja na kufanya vipimo kwa weledi ili kutoa majibu sahihi ambayo yataenda kuisaidia jamii badala ya kuiletea madhara”. Amesema Dkt. Saitori 


Kwa upande wake Msajili wa Baraza la Wataalam wa Maabara Bi. Mary Mtui wakati akizungumza na watarajali hao amewasihi kufuata taratibu na miongozo iliyopo katika vituo vya mafunzo.


"Nawasihi sana mnapoenda kwenye mafunzo jambo kubwa mnalotakiwa kulifanya ni kufuata taratibu na miongozo iliyopo katika vituo vyenu vya mafunzo ili muweze kujifunza mambo mengi kwa kipindi hicho cha Mwaka mmoja”. Amesema Bi. Mary 


Ikumbukwe kuwa, Mafunzo hayo elekezi kwa wataalam Watatajali wa Maabara yalihusisha Miiko na Maadili ya Taaluma, Mwongozo wa mafunzo ya utarajali, Sheria ya Wataalam wa Maabara pamoja na Kanuni za utumishi wa Umma.