Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WANANCHI WA CHIKONJI WAPONGEZWA KWA UTHUBUTU

Posted on: July 25th, 2025

Na WAF, Lindi

Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI imewapongeza wananchi na uongozi wa Kijiji cha Chikonji kilichopo mkoani Lindi kwa juhudi zao za kujitolea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha huduma za afya, hususan kwa kuanzisha ujenzi wa jengo la wodi ya uzazi kwa ajili ya akinamama na watoto.

Pongezi hizo zimetolewa Julai 24, 2025 na Bi. Faraja Mgeni, Afisa kutoka Idara ya Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto , Wizara ya Afya, wakati wa ziara ya ufuatiliaji na usimamizi shirikishi wa utekelezaji wa Mradi wa Ukarabati wa Vituo vya Afya unaofadhiliwa na Taasisi ya Susan Thompson Buffett Foundation (STBF), Mradi huo unalenga kuboresha huduma za afya ya uzazi kwa akinamama na watoto wachanga.

Bi. Faraja ameeleza kuwa wananchi wa Chikonji walichangisha Shilingi Milioni 4 kwa ajili ya kuanzisha ujenzi wa wodi hiyo kutokana na changamoto walizokuwa wakikabiliana nazo ambapo pia Halmashauri nayo ilichangia Shilingi Milioni 4, hivyo kuwezesha kuanza kwa ujenzi huo.

“Wananchi walijichangisha Shilingi Milioni 4, na Halmashauri ikatoa Milioni 4 nyingine jumla ikawa Milioni 8 ndizo fedha zilizoanzisha ujenzi huu, sasa fedha kutoka STBF zitasaidia kumalizia ujenzi huu ulipoishia,” amesema Bi. Faraja.

Aidha, Bi. Faraja amebainisha kuwa ufuatiliaji unaofanywa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI unalenga kuangalia hatua zilizofikiwa katika ngazi ya mkoa, halmashauri na vituo vya afya vilivyopokea fedha, pamoja na kutoa maelekezo ya namna ya kufanikisha utekelezaji wa miradi hiyo.

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mjini ambaye pia ni Afisa Miradi wa wilaya hiyo, Dkt. Charity Ngezi, amesema kuwa Kituo cha Afya cha Chikonji kilishapokea fedha kwa ajili ya ukarabati na kwamba ukarabati huo utakamilika kwa wakati.

“Tulifanya kikao na wananchi mara baada ya kupokea fedha hizo na kuwaeleza kuhusu mradi utakaoanza. Wananchi walifurahia sana na kuona kwamba changamoto ya huduma za uzazi kwa akinamama imepata ufumbuzi,” amesema Dkt. Ngezi