Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAMILIKI VITUO BINAFSI WATAKIWA KUSIMAMIA UBORA WA HUDUMA ZA AFYA

Posted on: February 2nd, 2024

Na WAF - DAR ES SALAM

Bodi ya ushauri hospital binafsi PHAB yatoa rai kwa Wamiliki, Mashirika yanayomiliki vituo Binafsi kuhakikisha yanasimamia ubora wa huduma za Afya, kuzingatia Sheria, Kanuni na miongozo ya Wizara ya Afya.

Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu wakati akitoa taarifa fupi kwenye kikao cha Bodi ya kumi ya bodi ya ushauri Hospitali binafsi Januari 2, 2024 Jijini Dar es salaam ambapo amesema ni muhimu kuhakikisha Watumishi wote ikiwemo, Madaktari, Wauguzi, Wataalam wa maabara, Wafamasia na Wataalamu wa radiolojia wanatambulika na kusajiliwa na Mabaraza yao na kuwa na leseni zilizo hai ili kuwaruhusu kutoa huduma za Afya kwa Wananchi.

"Kuna baadhi ya wamiliki wa vituo binafsi wanakiuka Sheria na Miongozo ya utoaji wa huduma za afya, mfano kutokuwa na Miundo Mbinu iliyokidhi, watumishi wasio na sifa na pungufu kulingana na ikama ya kituo pamoja na vifaa na vifaa tiba visivyotosheleza kulingana na ngazi ya kituo hivyo Bodi inatoa rai kwa Wamiliki na Mashirika yanayomiliki Vituo Binafsi kuhakikisha wanasimamia ubora wa huduma za Afya kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo ya Wizara ya Afya" amesema Prof. Nagu.

Prof. Nagu ameongeza kuwa nia ya Bodi ya ushauri hospital binafsi PHAB ni kuhakikisha sekta binafsi ya Afya inakua na kuzidi kusaidia Serikali katika kuimarisha Afya za Wananchi wake.

"Serikali inashukuru kwa uwekezaji mkubwa unaofanywa na Watu Binafsi katika Sekta ya Afya, Hadi sasa kuna jumla ya Vituo vya kutolea huduma za Afya takriban 10,286 na kati ya hivyo, Vituo 7,231 asilimia 58 ni vya Umma na vituo 3,185 sawa na asilimia 42 ni vya Binafsi. Ninavitaka Vituo Binafsi vyote ambavyo havijasajiliwa na vile ambavyo muda wa usajili umeisha waendelee na zoezi la kuhuisha vituo hivyo ili viweze kutambulika na Bodi hii" alimaliza Prof. Nagu.

Pia Prof Nagu amewakumbusha Watumishi wa Afya wa Serikali na Binafsi kufanya kazi kwa weledi, kutumia lugha zenye staha, kutunza siri na kuheshimu utu wa Wagonjwa wanaowahudumia.
MWISHO.