Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAHUDUMU NGAZI YA JAMII WASAIDIA KUPUNGUZA VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI NA MAAMBUKIZI YA MAGONJWA YA MLIPUKO MKOANI SIMIYU

Posted on: February 22nd, 2024



Na WAF - SIMIYU

Naibu katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe amepongeza juhudi za Mkoa wa Simiyu kutumia Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii 3,165 kusaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na magonjwa ya Mlipuko ikiwemo Kipindupindu.

Dkt. Magembe amesema hayo Februari 22, 2024, Mkoani Simiyu wakati akiendelea na na Ziara ya kukagua miradi ya ujenzi katika hospitali za Rufaa za Mikoa na kukagua utoaji wa huduma za afya kuanzia ngazi ya msingi hadi rufaa.

“Tumeona hapa kwa takwimu namna ambavyo wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii wamekuwa wakifuatilia wajawazito hadi majumbani na kuhakikisha wanahudhuria kliniki zao mapema kabla ya wiki ya 12 na kuchangia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 50 (2019) Hadi vifo 33 (2023) kwa Mkoa wa Simiyu” amesema Dkt Magembe

Dkt. Magembe amesema kupitia wahudumu hawa, serikali kwa kushirikiana na jamii wataweza kupunguza gharama za kuwatibu watanzania kwa sababu watagundulika kuwa na magonjwa wakiwa katika hatua za awali.

“Wahudumu hawa wameanza kuonyesha mafanikio makubwa wakati tukijiandaa na Utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa wahudumu wa afya ngazi ya Jamii ambao ulizinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt . Philip Mpango tarehe 31.01.2024.

Kuhusu kudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu, wahudumu hao wameonyesha namna walivyosaidia kuielimisha Jamii kuhusu usafi wa mazingira, elimu ya kujenga na kutumia vyoo Bora, kunawa mikono kila baada ya kutoka chooni na kabla ya kula, kugawa dawa za kutibu maji (AquaTabs) ngazi ya kaya na hivyo kupunguza kasi ya maambukizi ya ugonjwa huo.