Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

VITUO VIPYA 485 VYA KUTOA HUDUMA ZA AFYA VIMEONGEZEKA KWA MWAKA 2023

Posted on: January 10th, 2024

Na. WAF - Dar es Salaam


Vituo vipya 485 vya kutolea huduma za Afya vimeongezeka kutoka vituo 8,881 Disemba 2022 na kufikia vituo 9,366 Disemba 2023 sawa na ongezeko la asilimia 5.5 ikiwa ni mafanikio makubwa katika Sekta ya Afya.


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Januari 10, 2024 wakati akitoa taarifa ya hali ya utoaji huduma za Afya nchini kwa mwaka 2023 katika mkutano wake na Waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya Jijini Dar es salaam.


Amesema, Mgawanyo wa vituo hivyo vipya vya kutoa huduma za Afya hadi kufikia Disemba 2023 ni pamoja na Zahanati – 7,804 (83.3%), Vituo vya Afya – 1,126 (12.02%), Hospitali za Halmashauri – 171 (1.83%), Hospitali zenye hadhi ya Wilaya -180 (1.92%).


Pia, Hospitali za Rufaa za Mikoa – 28 (1.3%), Hospitali zenye hadhi ya Mkoa- 34 (0.36%), Hospitali za Rufaa za Kanda – 5 (0.05%), Hospitali zenye hadhi ya kanda- 11 (0.12%), Hospitali Maalumu – 6 (0.06%), Hospitali ya Taifa – 1 (0.01%).


“Ongezeko la vituo vya kutoa huduma za afya nchini limetuwezesha kusogeza huduma za Afya karibu zaidi na wananchi kama tunavyoelekezwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 - 2025.” Amesema