Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

VITANDA VYA WAGONJWA VIMEONGEZEKA KUFIKIA 126,209 MWAKA 2023

Posted on: January 10th, 2024


Na. WAF - Dar es Salaam


Idadi ya vitanda vya wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma za Afya nchini imeongezeka kufikia 126,209 Mwaka 2023 kutoka 104,687 mwaka 2022 ikiwa ni ongezeko la vitanda 21,522.


Waziri wa Afya Mhe. @ummymwalimu amesema hayo jana Januari 10, 2024 wakati akitoa taarifa ya hali ya utoaji huduma za Afya nchini kwa mwaka 2023 katika mkutano wake na Waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya Jijini Dar es salaam.


“Kwa kuzingatia idadi ya watu wa Tanzania bara, uwiano wa vitanda kwa idadi ya watu ni sawa na vitanda 2.1 kwa kila watu 1000 ambapo kwa mujibu wa viwango vya WHO kwa kila watu 1000 uwiano ni vitanda 2.5.” Amesema Waziri Ummy


Waziri Ummy amesema ongezeko la vitanda vya wagonjwa limesaidia kuongeza ubora na ufanisi wa huduma za Afya hususani huduma za Afya ya uzazi, mama na mtoto.


Aidha, Waziri Ummy amesema Disemba 2022 kulikuwa na vitanda vya Wagonjwa mahututi (ICU) 528 hadi kufikia Disemba 2023 vitanda vya Wagonjwa mahututi (ICU) vimeongezeka kumefikia 1,000.


“Wagonjwa wanaohitaji huduma za uangalizi maalumu (ICU) kwa sasa wanapata huduma hiyo kwa urahisi ukilinganisha na miaka ya nyuma.” Amesema Waziri Ummy


Amesema, ongezeko la vitanda vya wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali za umma linalenga kuboresha huduma na kupunguza vifo vinavyotokea ndani ya hospitali ambavyo vinaweza kuzuilika kwa kiwango cha asilimia 20 hadi 30.


“Mfano katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa walikuwa na Vitanda 8 (mwaka 2021) ambapo hadi mwaka 2023 vitanda vimeongezeka kufikia 20 (Mwaka 2023).” Amesema Waziri Ummy