Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

UJUMBE WA HELEN KELLER WAFIKA KITUO CHA AFYA ISMANI KUJIONEA ZOEZI LA HUDUMA YA UPASUAJI MTOTO WA JICHO

Posted on: August 6th, 2025

Ujumbe wa Bodi ya Shirika la Kimataifa la Helen Keller tarehe 5 Agosti, 2025 pamoja na masuala mengine ulifika Isman wilaya ya Iringa kujionea kwa vitendo zoezi linaoendelea la kambi ya upasuaji wa ugonjwa wa macho ujulikanao kama mtoto wa jicho kambi itakayotoa  huduma hiyo kwa siku saba. 


Akizungumza wakati wa kikao kifupi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa mkoani Iringa kabla ya kutembelea kituo hicho, Rais wa shirika hilo  Bi. Sarah Bochie amesema shirika hilo limeamua kutembelea mkoani Iringa ili kujionea na kujiridhisha na huduma zinazotolewa kwa vitendo kwani shirika lake linafanya kazi kwa kanzi data na takwimu ili kutoa tathimini ya huduma zake.


Kambi hiyo ya upasuaji mtoto wa jicho inaendelea kwa siku ya nne sasa na inafanya upasuaji wa mtoto wa jicho kwa takribani wagonjwa 120 kwa siku katika zoezi linaloendeshwa na Madaktari Bingwa kutoka hospitali za nyanda za juu kusini ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya.


Awali Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Kheri James wakati akikaribisha ujumbe wa Bodi ya Wataalam kutoka Helen Keller Ofisini kwake ameshukru shirika la Helen Keller kwa kutoa msaada wa vifaa kila vinapohitajika, kutoa utaalam kwa madaktari wenyeji na kuendeleza ushirikiano kati yao na serikali. 


Aidha Mhe. Kheri James amesema lengo la ujumbe wa Helen Keller Mkoani Iringa ni kujionea namna gani huduma wanazofadhili zinavyofanya kazi ikiwemo kujadiliana kwa pamoja maeneo mengine ya ushirikiano kwani shirika hilo limekuwepo hapa nchini kwa zaidi ya miaka 30.



Kufuatia uwepo wa zoezi hilo katika Kituo cha Afya Ismani idadi kubwa ya wanachi wenye shida ya tatizo la mtoto wa jicho imeendelea kujitokeza ili kupata tiba hiyo huku wagonjwa wengi wenye umri wa miaka 50 na kuendelea wakiwa wanaongoza kwa kuwa na uoni hafifu hivyo kufanya idadi kubwa ya watu wenye umri mkubwa kufanyiwa upasuaji kwa wingi.


Dkt. Stephen Nyamsae Daktari Bingwa wa macho amesema ugonjwa wa mtoto wa jicho ni ukungu unaotokea katika kioo cha ndani ya jicho kutokana na kuongezeka kwa umri hasa kwa watu wenye umri zaidi ya miaka 50 ambao taratibu hupoteza uwezo wa kuona.


Dkt. Nyamsae anayataja makundi mengine kuwa ni watoto wanaozaliwa na mtoto wa jicho kutokana kioo  hushindwa kujitengeneza kabla ya kuzaliwa, kundi lingine analitaja kuwa ni la watu wenye ugonjwa wa kisukari lakini pia watu wanaopata majeraha katika jicho kutokana na ajali.    

Zoezi la Kambi ya Upasuaji wa mtoto wa jicho linaendelea kwa siku saba (7) likitarajia kuhitimishwa Agosti 9, 2025, hivyo amewataka wananchi waendelee kujitokeza kutumia fulsa hii kwani huduma hii inatolewa bure na imedhaminiwa na shirika la kimataifa lisilo la kiserikali la Helen Keller.