Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

UGONJWA WA HOMA YA MGUNDA UMEDHIBITIWA

Posted on: July 29th, 2022

Na. WAF - Dar es Salaam 


Ugonjwa wa homa ya Mgunda (Leptospirosis) ambao ulithibitishwa kimaabara nchini Julai 18, 2022 na kutolewa taarifa kwa umma kuwepo kwa ugonjwa huo umedhibitiwa.


Hayo ameyasema Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo Julai 29, 2022 alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam .


"Hadi kufikia asubuhi ya leo Julai 29, 2022 idadi ya wagonjwa waliothibitishwa kuugua ugonjwa huo nchini ni 20 na kati yao watatu wamefariki."amesema Waziri Ummy 


Aidha Waziri Ummy amesema wagonjwa wote waliyolazwa wameruhusiwa kurudi nyumbani na wanaendelea na majukumu yao kama kawaida.


"Ugonjwa huu unatibika kwa kutumia dawa ambazo zinapatikana katika vituo vya kutolea huduma za Afya kote nchini."amesema Waziri Ummy 


Sambamba na hilo Waziri Ummy amebainisha kuwa miongoni mwa watu waliotangamana na wagonjwa hao (Contacts) hakuna aliyeonesha dalili za ugonjwa huo hadi kufikia sasa.


Pia, amesema hii inadhihirisha kuwa ni mara chache ugonjwa huu huambukizwa kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa mwingine. 


Hata hivyo, wataalamu wanaendelea na utafiti wa kina kwa binadamu, wanyama, na mazingira yanayowazunguka ili kubaini na kuweka mikakati ya kudhibiti ugonjwa huu nchini.


Wizara ya Afya inaendelea kusisitiza kwa wananchi waendelee kuchukua tahadhari zote stahiki za kujikinga na ugonjwa huo ikiwemo kuepuka kutumia maji au vitu vilivyochafuliwa na mkojo wa wanyama pia kunywa maji safi ambayo yamechemshwa au kutibiwa.


Kumbuka kuwa, Dalili za ugonjwa wa homa ya Mgunda (Leptospirosis) ni pamoja na homa, kuumwa kichwa, maumivu ya misuli, uchovu wa mwili, mwili kuwa na rangi ya manjano, macho kuvilia damu, kutoka damu puani, kukohoa damu, kichefuchefu na kuharisha. 


Mwisho, Waziri Ummy amewataka wananchi wahakikishe wanafika kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya mapema ili wapate uchunguzi na matibabu sahihi, Pia, kutoa taarifa pindi wanapoona dalili za ugonjwa huo.