Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TANZANIA NA WANA-DIASPORA KUENDELEA KUSHIRIKIANA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA NCHINI

Posted on: January 13th, 2024


Na. WAF - Dar es Salaam


Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Afya iko tayari kuzidisha mashirikiano na Wana-Diaspora ili kuendelea kuboresha upatikanaji wa Huduma za Afya kwa Watanzania.


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Januari 13, 2024 wakati wa mkutano wake na Watanzania wanaofanya kazi katika Sekta ya Afya nchini Uingereza uliofanyika kwa njia ya mtandao.


Waziri Ummy amesema lazima kuwepo na dawati maalumu litakaloratibu mawasiliano na uhusiano baina ya Wizara ya Afya na Diaspora ambalo litakuwa chini ya Mganga Mkuu wa Serikali.


“Tunahitaji kuangalia namna gani tunaweza kuvutia wadau ambao wako tayari kufanya uwekezaji nchini katika kuongeza vituo vya kutoa huduma za Afya pamoja na maabara zitakazoweza kufanya vipimo maalumu. Amesema Waziri Ummy.


Amesema, Serikali imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha huduma za Afya zinasogezwa karibu zaidi na wananchi kwa kufanya maboresho ya ujenzi wa Hospitali katika ngazi mbalimbali, upatikanaji wa Vifaa pamoja na Vifaa Tiba vya kisasa.


“Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa tutupatia Tsh. Bilioni 8 kwa jili ya kupeleka wataalam kwenda kupata mafunzo nje ya nchi kwa Seti na sio mmoja mmoja kama ilivyokuwa awali.” Amesema Waziri Ummy


Mwisho, Waziri Ummy amewashukuru na kuwapongeza Wana-Diaspora kwa kazi nzuri wanazozifanya kwa kushiriana na Hospitali zilizopo nchini Tanzania ikiwemo Hospitali ya Tumbi, Hospitali ya Mnazi mmoja pamoja na MOI.