Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TANZANIA NA UTURUKI KUANZA UTEKELEZAJI WA MKATABA WA MASHIRIKIANO SEKTA YA AFYA

Posted on: August 9th, 2022

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi na Naibu Waziri wa Afya wa Uturuki Dkt. Tolga Tolunary wamekutana na kufanya mazungumzo ya namna ya kuanza mara moja utekelezaji wa Mkataba wa mashirikiano katika sekta ya afya yaliyosainiwa mwaka 2017.

Majadiliano hayo yamefanyika Leo tarehe 8/8/2022 katika ofisi za Wizara ya Afya jijini Ankara, Uturuki.

Maeneo mbalimbali ya ushirikiano yalijadiliwa ikiwemo mafunzo ya kibingwa na ubingwa ubobezi kwa wataalamu wa kada mbalimbali za Afya, matibabu yasiyopatikana nchini Tanzania, uwekezaji wa Hospitali, viwanda na vifaa tiba nchini Tanzania, mageuzi ya mfumo wa TEHAMA wa taarifa za afya za wananchi wote unavyotumika nchini humo.

Katibu Mkuu pamoja na ujumbe aliombatana nao walipata fursa ya kuelezwa kuhusu mageuzi yaliyofanyika kwa miaka ishirini sasa katika mfumo wa sekta ya afya na uendeshaji wa bima ya afya kwa wote unavyotekelezwa nchini Uturuki.

Aidha, uzoefu ulitolewa wa matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika kuwa na e-Database ya wagonjwa wote nchini humo, utunzaji na usafirishwaji wa kumbukumbu zao (vipimo, magonjwa, dawa) kutoka hospitali moja kwenda hospitali nyingine na utambuzi, ufatiliaji(tracking) na udhibiti wa dawa katika supply chain kuanzia ngazi ya utengenezaji/uingizaji mpaka kwa mlaji (mgonjwa).

Vilevile, Katibu Mkuu na ujumbe wake walielezwa kuhusu mfumo unaotumiwa na Wizara ya afya kwenye huduma za dharura na majanga ambapo magari yote ya dharura yanaratibiwa kutoka vituo mbalimbali katika kituo kikuu kilichopo wizarani pamoja na uwepo wa mfumo unaofuatilia magari ya kubeba wagonjwa (ambulances) nchi nzima.

Viongozi hao walikubaliana kuundwa kwa kamati maalum ya kiutendaji itakayoratibu makubaliano yaliyofikiwa na kuweka mfumo wa tathimini na ufuatiliaji wake.

Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu pia aliambatana na Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Uturuki Mhe. Hassan Mwamweta na kutoa salaam za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu kwa Serikali ya Uturuki.