Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TANGA, KAGERA ZAPOKEA MIZANI KUFUATILIA MAENDELEO YA AFYA YA MAMA NA MTOTO

Posted on: August 5th, 2025

Wizara ya Afya imekabidhi mizani ya kupimia uzito kwa mtoto na mama mjamzito kwa mikoa ya Tanga na Kagera ikiwa ni sehemu ya kuongeza jitihada za kuweka mazingira rafiki ya kutambua maendeleo ya afya kwa mama mjamzito na mtoto aliyezaliwa.


Mizani hiyo imekabidhiwa na Mkurugenzi wa Huduma za Lishe Wizara ya Afya Bi. Neema Joshua  leo Agosti 5, 2025 katika Wiki ya Maadhimisho ya unyonyeshaji yanayofanyika kitaifa Jijini Dodoma.


Bi. Neema  amesema mizani  hiyo ni miongoni mwa juhudi za Serikali katika kuboresha afya na kujenga mhimili bora wa jamii kwa kulinda afya za wajawazito na watoto wadogo nchini.



Kiongozi huyo wa Wizara ya Afya amesema  zoezi hilo linapaswa kuigwa na Halmashauri zote nchini, kwani mizani inapokuwa mingi ni rahisi kujua maendeleo ya mtoto, lishe anayopata na afya yake kwa ujumla. 


“Upatikanaji wa mizani katika vituo vya afya ni jitihada zetu kulinda afya ya mama mjamzito na mtoto, ni msingi wa kujenga jamii imara na tunazihimiza Halmashauri zote nchini kuiga hatua hii, kwani kadri mizani inavyoongezeka, tunaweza kufuatilia kwa urahisi maendeleo ya lishe na afya ya watoto.” amesema  Bi. Joshua.



Naye  Mkurugenzi wa Ushirikiano na s

Sera Afrika Mashariki Bw. Gwao Omari, amesema matumizi ya teknolojia mpya katika kufuatilia na uzalishaji wa unga wa mahindi na ngano inaleta ubora wa virutubisho vyenye tija kwa afya ya mama na mziwa yaliyo na lishe kubwa kwa mtoto.


Amesema, sekta binafsi inashirikiana kwa karibu na wataalam wa lishe kutoka Halmashauri za 

Serikali za Mitaa ambapo makubaliano yamefikiwa kuhakikisha kuwa wataalam hao wanatoa elimu kwa jamii na kusimamia usindikaji wa vyakula, huku sekta binafsi zikitoa vifaa vya kiteknolojia na kiufundi vinavyowezesha ufuatiliaji wa hali ya lishe na uzalishaji wa chakula.


Maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji yanayoadhimishwa kila mwaka duniani kati ya Agosti 1-7  yamedhamiria  kupeleka elimu zaidi kwa jinsia zote ikiwemo akina baba ambao kwa kiwango kikubwa wanahusika kwenye kuboresha lishe ya mama na mtoto.