Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI, WHO KUTOA MWONGOZO WA MALEZI YA WATOTO NA VIJANA RIKA BALEHE KATIKA JAMII

Posted on: October 8th, 2025

Na WAF, Dodoma. 


Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani WHO inatarajia kutoa  mwongozo wa malezi na makuzi kwa Watoto pamoja na vijana rika balehe ili kuboresha afya zao.



Serikali itakuja na mwongozo huo utakaondaliwa kwa pamoja na  Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii  pamoja  na Shirika la Afya Duniani(WHO).


Hayo yamebainishwa  leo  Oktoba 08, 2025  na Afisa Program wa Mpango wa Taifa wa Afya na Lishe wa Wizara ya Afya Dkt. Lilian Lyatura, wakati wa Kikao kazi  cha siku mbili cha  kupitia Mwongozo huo kinachoendelea Jijini Dodoma.


Aidha Dkt. Lyatura amesema Uandaaji wa vielelezo vya Uelimishaji kuhusu masuala ya Malezi na Makuzi kwa Watoto pamoja na vijana wa rika balehe utasaidia watoa huduma za Afya katika vituo vya kutolea huduma, wazazi pamoja na walezi waweze kuwa na uelewa wa pamoja juu ya masuala ya malezi na usimamizi wa makuzi ya vijana na rika balehe katika Jamii.


"Mwongozo huu ni muhimu kwani utasadia kutoa elimu kwa watoa huduma za Afya, Wazazi na Walezi jinsi ya kutambua dalili hatari za mwanzoni kwa watoto na vijana ili kuimarisha afya, malezi na makuzi bora kwa watoto na vijana," amesema Dkt.amesema Dkt. Lyatura.


Kikao kazi hicho  pia kitaandaa Kitita cha Mwongozo  wa Malezi pamoja na Kuandaa Mpango wa kufanya mafunzo na majaribio ya awali kwa watoa huduma za Afya, Waratibu wa Huduma za Mama na Mtoto pamoja na Waratibu wa Elimu ya Afya kwa Umma kwa ngazi za mikoa na halmashauri.