Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERA YA LISHE KUBORESHWA - WAZIRI UMMY MWALIMU

Posted on: October 2nd, 2022

Na WAF - Dodoma.

Serikali kupitia Wizara ya Afya pamoja na wadau wa Sekta ya Afya wamepanga kuendelea kushirikiana katika kuboresha Sera ya Lishe na kutekeleza afua za lishe nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu Leo kwenye Hafla ya kusaini Mkataba wa Lishe kati ya Rais Samia Suluhu Hassan na Wakuu wa Mikoa.

“Tutaendelea na jukumu la kuandaa na kutoa Sera, Miongozo na Mikakati ya Afya ikiwemo huduma za Lishe, tumepokea malekezo yako Sera ya Lishe imepitwa na wakati tutalifanyia kazi” amesema Waziri Ummy Mwalimu

Katika kupunguza udumavu kwa watoto Waziri Ummy amesema kuwa Serikali itaendelea ku shirikiana na Wadau wa lishe nchini kutekeleza afua zitakazoleta matokeo makubwa zinazolenga Siku 1000 za maisha ya mtoto.

Ametaja afua hizo kuwa ni pamoja na kutoa matone ya madini ya chuma na asidi ya ‘folic’ kwa wakina mama wajawazito takribani Milioni 2.3 kwa mwaka, kutoa matone ya Vitamini A, Dawa za kutibu Minyoo ya tumbo mara mbili kwa Mwaka kwa watoto wote wenye umri wa chini ya miaka 5.

Waziri Ummy amesema Serikali itaendelea kutoa matibabu ya utapiamlo mkali kwa watoto walio chini ya miaka 5, kutoa elimu ya ulaji wa vyakula mchanganyiko na mtindo bora wa maisha unaolenga kuondokana na tabia bwete.

“Chini ya usimamizi wa Ofisi ya Waziri mkuu, Sekta zote mtambuka zitaendelea kushirikiana kutekeleza Mpango Kazi Jumuishi wa pili wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Afua za Lishe (National Multisectoral Nutrition Action Plan- NMNAP II 2020/21)” amesema Waziri Ummy.

Hata hivyo Waziri Ummy amesema Serikali imefanikiwa kupunguza utapiamlo na ukondefu kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano kutoka asilimia 4.5 (2015/16) hadi 3.5% (2018) ikiwa takribani watoto laki 6 huku akibainisha kuwa kazi bado iko kubwa kuelimisha jamii kuhusu Lishe bora.

Mwisho