Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA WAREJESHA MATUMAINI MAGONJWA YA KOO PUA NA SIKIO KWA WATOTO KAGERA

Posted on: May 9th, 2025

Kambi ya Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia ianayoendelea Mkoani Kagera imetoa tiba kwa watoto wapatao 149 hadi sasa waliokuwa wakisumbuliwa na magonjwa ya koo, pua pamoja na masikio.

Dkt. Bingwa wa Magonjwa ya Pua, Koo pamoja na Masikio Dkt. Pius Lema akizungumza kuhusu zoezi hilo Mei 7, 2025 amesema kati ya wagonjwa hao 19 tayari wamefanyiwa upasuaji na idadi hiyo itaongezeka kwakuwa wagonjwa wanaendelea kujitokeza na kupatiwa huduma.

Dkt. Lema amesema dalili za ugonjwa huo kwa watoto ni pamoja na kukoroma nyakati za uzingizi, kupiga chafya kila mara, kushutuka usingizini na kulala mdomo wazi na amewataka wazazi na walezi kila waonapo watoto wenye dalili hizo kuwapeleka watoto wao hospitali kwa ajili uchunguzi.

Mbali na matibabu ya koo, pua na sikio Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Mifupa wamefanikiwa kurejesha furaha ya mgonjwa ambaye alipata changamoto ya ajali na kuvunjika mwaka mmoja uliopita lakini suluhisho la ugonjwa wake limepata tiba baada ya ujio wa timu ya madaktari wabobezi mkoani Kagera.

Kufuatia tiba hiyo Bi. Devota Kaigwa Mkazi wa Kijiji cha Kalabagaine amerejesha furaha yake baada ya kufanyiwa upasuaji na kupata matumaini mapya baada ya tatizo lake kupatiwa ufumbuzi na kusifu juhudi za Rais Samia za kuleta Mabingwa hao.

Naye Mzee Humud Abdallah mwenye umri wa miaka 84 mkazi wa Kyaka ametoa shukurani kwa Rais Samia kuwezesha kambi hiyo mkoani Kagera kwani amepatiwa nafuu kubwa ya ugonjwa ambao umekuwa ukimsumbua kwa miaka saba sasa.

“Nashukru sana kwakuwa siwezi kusema kwamba nimehudumiwa vibaya, tiba ni nzuri na uvimbe katika miguu yangu umeanza kupungua, nawashauri Watanzania wenzangu kufika hapa ili kupatiwa tiba,”amesema Mzee Abdallah.

Kambi ya Madaktari Bingwa ya huduma za Mkoba ya Rais Samia inaendelea kwa siku ya nne mkoani Kagera kwa ngazi ya Hospitali ya Rufaa na itakamilisha kazi yake Mei 9, 2025 huku watu wakiendelea kujitokeza kwa wingi kupata huduma hiyo.