Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA WAFANYA MAKUBWA GEITA, TANGA, MOROGORO NA RUVUMA.

Posted on: April 30th, 2024



Na WAF

Madaktari Bingwa na Bobezi wa Rais Samia wanao kwenda na kauli mbiu imesemayo “Tumekufikia Karibu Tukuhudumie” wameanza kwa kufanya mambo makubwa kwa Mikoa ya Geita, Tanga, Ruvuma na Morogoro kwa kubadilishana uzoefu, ujuzi ambao umeongeza tija na ufanisi katika utendaji wa kazi kwa madaktari wegine.

Wakizungumza kwa Nyakati tofauti wamesema, kambi ya Madaktari Bingwa iliyoanza Aprili 29, 2024 imewawezesha madaktari kubadilishana uzoefu pamoja na kutatua changamoto za wagonjwa kwa wakati.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Mifupa Mkoani Geita Dkt. Zablon Saguta amesema ndani ya siku Moja (Aprili 30, 2024) wamekutana na wananchi wenye shida ya mifupa wapatao 70 ambapo Idadi hiyo itaweza kuongezeka kutokana na wananchi kuendelea kupata taarifa ya ujio wa madaktari hao.

Akifungua kambi hiyo mkoani Tanga, Mkuu wa Mkoa wa huo Balozi Dkt. Batilda Buriani amesema madaktari Bingwa na Bobezi wa Rais Dkt. Samia zaidi ya 30 wamefika Mkoani humo kusaidiana na madaktari 60 waliopo ambapo watu zaidi ya 700 wamejitokeza na kupatiwa huduma za matibabu.

Taarifa kutoka Nyanda za Juu Kusini iliyokita kambi Mkoani Ruvuma inasema zaidi ya wananchi 3,500 wenye changamoto za magonjwa mbalimbali wa Mkoa huo na maeneo ya jirani nao wamejitokeza kwenye huduma za Kibingwa na Ubingwa Bobezi.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima walati akiongea na waandishi wa habari kuelekea zoezi hilo katika Mkoa huo amesema Madaktari Bingwa na Bobezi 56 wanatarajia kushiriki kutoa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi kwa wananchi zaidi ya 2000 wa Mikoa ya Morogoro, Iringa, Singida, Dodoma na Pwani kupitia kambi maalum ya matibabu ya siku Tano ndani ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kuanza tarehe 6 Hadi 10 Mei, 2024.

Miongoni mwa magonjwa yatakayotolewa huduma katika kambi za madaktari Bingwa na Bobezi ni pamoja na magonjwa ya akina mama na uzazi, magonjwa ya ndani kama vile shinikizo la damu, Kisukari, Figo, magonjwa ya watoto, mifupa, upasuaji, macho, kinywa na meno, pua na koo, upasuaji wa watoto wenye midomo sungura, masikio, ngozi, moyo, mfumo wa chakula pamoja na magonjwa ya Saratani.