MABORESHO MAKUBWA YAFANYIKA CHUMBA CHA UPASUAJI WATOTO HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA MBEYA
Posted on: May 6th, 2025
Na WAF, Mbeya
Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya leo imefanya uzinduzi wa ufunguzi wa huduma za chumba cha upasuaji wa watoto (Pediatric Operating Theatre) baada ya kufanyiwa maboresho makubwa ya mwonekano na kuwekewa vifaa tiba vya kisasa.
Maboresho hayo yamefanyika kwa ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Smile Train kutoka Marekani linaloratibu matibabu ya mdomo wazi na shirika la Kids Operating Room (KidsOR) kutoka nchini Scotland linalojitolea kuboresha huduma za afya ya watoto kupitia uwekezaji kwenye miundombinu ya upasuaji.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mei 6, 2025 Mkoani Mbeya, Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali Dkt. Uwesu Mchepange amewashukuru wafadhili kwa msaada wao na kueleza namna maboresho hayo yatakavyoongeza ufanisi wa utoaji huduma za upasuaji kwa watoto.
Pia chumba hicho kina mazingira rafiki na ya kufurahisha kwa watoto wanaohitaji huduma za upasuaji yatakayosaidia kupunguza hofu na wasiwasi kwa watoto hao kabla na baada ya upasuaji.
Dkt. Mchepange ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa nafasi kwa wadau wa maendeleo kushirikiana na Serikali ili kuboresha sekta ya afya nchini.
Kwa upande wake, Bi. Veronica Kimwela, Msimamizi wa Miradi ya Smile Train Tanzania na Bi. Jenn Perkison Mratibu wa KidsOR, ameshukuru hospitali kwa kutoa nafasi ya kushirikiana nao katika mradi huo muhimu na kuahidi kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na hospitali hiyo na taasisi nyingine za afya nchini kwa manufaa ya watoto wa Tanzania.
Ufunguzi wa chumba hiki cha upasuaji wa watoto kilichofanyiwa maboresho unatarajiwa kuongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya kutoa huduma bora za upasuaji kwa watoto kutoka Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na maeneo mengine ya jirani. Hii ni hatua kubwa katika kuboresha afya ya watoto nchini Tanzania.