Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MAAMBUKIZI YA VVU YAMEPUNGUA KUTOKA 7% MWAKA 2003/04 HADI 4.4% MWAKA 2022/23 KWA TANZANIA.

Posted on: February 6th, 2024

Na. WAF - Dar Es Salaam

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema kwa Tanzania maambukizi ya VVU yamepungua kutoka asilimia 7 mwaka 2003/2004 hadi kufikia asilimia 4..4 mwaka 2022/2023, kukiwa na tofauti kati ya watu na maeneo mbalimbali ya kijiografia.

Waziri Ummy amesema hayo leo Februari 6, 2024, jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa siku Mbili wa mapitio ya kimkakati wa PEPFAR COP muhula wa 23 kwa lengo la kutathmini hatua iliyofikiwa kuhusu mwitikio wa VVU katika kufikia udhibiti wa UKIMWI ifikapo mwaka 2030.

“kikao hiki kinalenga kujadili na kubainisha mikakati itakayowezesha ufanisi wakati wa utekelezaji wa afua za msingi na kubainisha ufanisi utakaowezesha kufikia malengo kabambe yaliyoainishwa katika sera na nyaraka za kimkakati za Nchi.” Amesema Waziri Ummy

Aidha, Waziri Ummy amesema kupaumbele katika masuala ya VVU/UKIMWI ni pamoja na kulinda mafanikio yaliyofanyika, kupunguza maambukizi mapya hususan kwa vijana balehe pamoja na kupunguza maambukizi mapya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Amesema, Tanzania imepiga hatua kubwa katika nyanja mbalimbali za mwitikio wa VVU ambapo kwa mujibu wa ripoti ya UNAIDS 2022, Tanzania imefikia Mkakati wa Kimataifa wa UKIMWI 2021 hadi 2026 kwa lengo la matibabu.

“Mafanikio haya yamechangiwa na matokeo ya Utafiti wa Athari za VVU Tanzania Mwaka 2022-2023 (HII 2022-2023) ambao uliripoti kufikiwa kwa malengo ya UNAIDS 95-95-95 kwa 82.7%, 97.9% na 94.3% (ngazi ya jamii).” Amesema Waziri Ummy

“Ikijumuisha 95% ya watu wanaokadiriwa kuwa na maambukizi ya VVU na wanafahamu hali zao za VVU, 95% ya walioambukizwa VVU na wanatumia dawa za kufunaza VVU (ARVs) na 95% ya wale wanaotumia ARVs walifikia hali ya kufunaza VVU.” Amefafanua Waziri Ummy

Mwisho, Waziri Ummy amewashukuru washirika wa Kimataifa wakiwemo PEPFAR, Global Fund, UNAIDS, WHO, UNICEF, CDC, USAID, DOD pamoja na Peace Corps kwa msaada usioyumba wa kiufundi na kifedha katika azma ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kumaliza janga la VVU na UKIMWI ifikapo mwaka 2030.