Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

KATIKA KILA WATU 100 WENYE SARATANI 25 NI WANAWAKE WENYE SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI

Posted on: February 4th, 2024

Na. WAF - Dar Es Salaam

Serikali imetoa rai kwa jamii kuchukua hatua za mapema kupima ugonjwa wa Saratani kwa kuwa takwimu zinaonesha kuwa katika kila wagonjwa watu 100 wenye Saratani 25 ni wanawake wenye Saratani ya Mlango wa Kizazi.

Hayo yamesemwa leo Februari 4, 2024 na Mkurugenzi wa Huduma za Afya na Ustawi wa Jamii kutoka OR - TAMISEMI Dk. Rashid Mfaume akimuwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu katika Maadhimisho ya Siku ya Saratani Duniani yaliyofanyika Jijini Dar Es Salaam.

“Ili kuepukana na Magonjwa hayo inatupasa tuwe na tabia ya kufanya mazoezi, kufuata mtindo bora wa maisha ikiwemo kuzingatia ulaji wa vyakula vyetu ili kuepuka magonjwa Yasiyoambukiza kwa kuwa kuna ongezeko kubwa la wagonjwa ambao asilimia kubwa ni wanawake.” Amesema Dkt. Mfaume

Amesema, Saratani inayoongoza ni ya Mlango wa Shingo ya Kizazi kwa wasatani kwenye kila wagonjwa wa 100 wa Saratani, wanawake 25 wana Saratani hiyo, nyingine ni Saratani ya Matiti lakini pia Saratani ya Koo ambapo takwimu zinaonesha kuwa katila kila wanawake 1,000 wanawake Sita wana Saratani hiyo.

Aidha, Dkt. Mfaume amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa aliyoufanya katika Sekta ya Afya ikiwemo kutoa zaidi ya Shilingi Bilioni 18 za ununuzi wa Vifaa Tiba katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI).

“Kutokana na uwekezaji mkubwa uliyofanyika kuna wagonjwa kutoka nchini Zambia, Comoro, Msumbiji, Burundi na Kenya ambao wanafika katika Taasisi hiyo ya ORCI kupata matibabu.” Amesema Dkt. Mfaume

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dkt. Julius Mwaisalage nae amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji huo anaoendelea kuufanya katika taasisi hiyo, ikiwemo ununuzi wa mashine ya kisasa ya uchunguzi wa Saratani.

“Maadhimisho haya ya siku ya Saratani Duniani mwaka huu yana kauli mbiu isemayo ‘Saratani inatibika huduma sawa kwa wote’ tuzingatie kauli hii kwa kufuata ushauri wa wataalamu katika kuzingatia mtindo bora wa maisha.” Amesema Dkt. Mwaisalage