Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA UTENDAJI WA MSD

Posted on: February 3rd, 2024

Na. WAF, Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Maswala ya UKIMWI imeitaka Bohari ya Dawa (MSD) kuongeza ufanisi, ubunifu wa hali ya juu kwa kuhakikisha dawa zinanunuliwa, zinahifadhiwa sehemu sahihi, kusambaza dawa hizo kwa wakati katika sehemu zenye uhitaji na kukusanya madeni ili kuweza kuwa imara na taasisi endelevu.

Wito huo umetolewa leo Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya na Maswala ya UKIMWI, Mhe. Stansilaus Nyongo baada ya kupokea taarifa ya hali ya utendaji na majukumu ya Bohari ya Dawa (MSD).

Mhe. Nyongo amesema kuwa wao kama wawakilishi wa wananchi wataendelea kuishinikiza serikali kuiwezesha MSD kupata mtaji ili kujiendesha kiufanisi katika kusambaza dawa kwa wakati.

“Bohari kuu ina majukumu ya kununua, kutengeneza, kuhifadhi dawa pamoja na kusambaza dawa katika vituo vya vyote nchini”. Ameeleza Mhe. Nyongo.

Mhe. Nyongo amesema kwa ujumla kamati imeridhishwa na hali ya utendaji wa Bohari ya Dawa na mipango yake ya utekelezaji wa majukumu yake ikiwemo uzalishaji wa dawa ili kupunguza kununua dawa nje ya nchi.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavele Tukai kwa uongozi imara katika taasisi hiyo na kufanya upatikanaji wa dawa kwa wakati kuongezeka nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavele Tukai amesema MSD ina mipango ya kuanzisha kampuni tanzu ambayo itaingia mikataba na makampuni binafsi ya ndani na nje katika kuwekeza viwanda vya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali za dawa na vifaa tiba nchini.